PAROKIA YA MWENGE


??

?HISTORIA YA PAROKIA YA MT. MAXIMILIA MARIA KOLBE MWENGE

1.0 UTANGULIZI
Hapo mwanzo, katika kipindi cha miaka ya 1969 na 1985, Parokia ya Mwenge ilizaliwa ndani ya jimbo Kuu la Dar es Salaam ikiwa mojawapo ya Parokia kumi na moja (11) zilizofunguliwa chini ya uongozi wa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa. Katika kipindi hicho, Parokia ya Mwenge ilianza mwezi Novemba 1973 kama Kigango chini ya usimamizi wa Parokia ya Mwananyamala. Kwa muda wa miaka minane (Nov. 1973 – Mei 1981), Baraza la Walei la Kigango liliwajibika kwa Halmashauri ya Parokia kwa mambo yote. Mwezi Mei 1981 Baba Askofu Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa alitoa idhini kwa Baraza la Kigango kuamua baadhi ya mambo na kuyawasilisha moja kwa moja kwenye Baraza la Walei Jimbo. Ndani ya miaka minne iliyofuata, Kigango kilipata hadhi ya kuwa Parokia mapema mwaka 1985.

Wakati Parokia ya Mwenge inazinduliwa mwaka huo 1985, iliwekwa chini ya usimamizi wa Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe ikiwa kwa wakati huo ni Parokia ya ishirini na moja (21) katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Jina la msimamizi wa Parokia lilipendekezwa na Paroko wa kwanza Mhe. Padre Zeno Zgudziak SDS kwa vile Mt. Maximilian Maria Kolbe alikuwa ametangazwa rasmi tarehe 10 Oktoba, 1982 na Baba Mtakatifu Papa Yohane Paulo wa Pili. Halmashauri Walei Parokia ilikubaliana na pendekezo hilo na kulipitisha kwa kauli moja.

2.0 KUANZISHWA KWA KIGANGO NA HATIMAYE PAROKIA

2.1 Kupatikana kwa kiwanja
Historia ya Mwenge yaweza kuchukuliwa kuwa ilianza mwaka 1973 pale ambapo Wakatoliki waliokuwa wamejiunga na Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge (Mwenge Housing Co-operative Society Ltd.) walipoanza kuhamia katika nyumba zao. Jumapili moja asubuhi mwaka 1973 baadhi ya Wakristo hao wa Mwenge Kijijini walisimama kituoni, Barabara ya Bagamoyo (sasa ni Ally Hassan Mwinyi) wakisubiri usafiri wa mabasi yaendayo Kawe, Kariakoo, au Stesheni ili waweze kuwahi popote kwenye kanisa kushiriki ibada ya Dominika. Bahati mbaya usafiri uliwatupa mkono siku ile, nao kwa uchungu walirudi nyumbani.

Kwa bahati nzuri, wakristo hao hawakukaa kimya kwani kutokana na matatizo kama hayo ya mara kwa mara, kikundi cha Wakatoliki wakereketwa walikutana katika nyumba ya Bwana Peter Masaiya hapo Mwenge Kijijini (Nyumba Na. 52/43) ili kujadili masahibu yao. Kwa pamoja walikubaliana kutuma ujumbe wa watu wawili kwenda kumwona Padre George Smith wa Parokia ya Mwananyamala ili aweze kutatua matatizo ya Wakristo wa Mwenge. Ujumbe huo ulishauriwa kuwasiliana pia na Mapadre wa Kawe na Chuo Kikuu wakati wakisubiri kujua Mwenge itawekwa chini ya uongozi wa Parokia ipi, kati ya Kawe, Chuo Kikuu na Mwananyamala. Ingawa juhudi za kwanza zilishaonekana kwa kuja kwa Padre kutoka Chuo Kikuu na kuadhimisha Ibada ya Misa chini ya Mkorosho, bado matatizo ya waamini hao yalibakia palepale. Ilitokea siku moja, Sista Ursula Hopfensitz SDS ambaye alikuwa akifundisha dini wanafunzi wa Kidato cha tano (V) na sita (VI) katika shule ya Aga Khan (sasa Mzizima) kusikia shida ya Wakristo wa Mwenge Kijijini, ambapo alimwomba mwanafunzi mmoja aitwaye Richard Nkwazi kufuatana naye hadi Mwenge ili aonane na viongozi wa Kamati iliyoteuliwa. Kwa pamoja walifanya majadiliano ya kutosha na Sista Ursula akaahidi kurudi tena Mwenge akiwa na Padre wa Mwananyamala.
Baada ya kujulikana Mwenge itakuwa chini ya Parokia ya Mwananyamala, Paroko Msaidizi wa Mwananyamala Padre Adelhem Grab, OSB, akifuatana na Sista Ursula Hopfensitz SDS walitembelea Mwenge tarehe 18 Novemba 1973 na kukutana na baadhi ya wakristo na kuzungumzia matatizo ya kukosa huduma za kiroho mahali hapo. Siku hiyo Padre Adelhem alisoma misa ya kwanza Mwenge na wakristo wapatao 55 walihudhuria.

Baada ya misa hiyo, Halmashauri ya kwanza ilikaa na Padre Adelhem Grab O.S.B. na kuchagua Kamati ya watu wanane (8) chini ya Uenyekiti wa Bwana Peter Masaiya ili isaidiane na Padre  kutafuta kiwanja cha kujenga kibanda cha kusomea misa na vilevile kusimamia na kuendeleza shughuli za dini katika eneo la Mwenge. Tarehe 24 Novemba 1973, Wajumbe wa Halmashauri wakiwa pamoja na Padre Adelhelm walijulishwa na kuonyeshwa eneo ambalo lilikwisha kutengwa na serikali kwa ajili ya shughuli za kidini. Idhini hiyo iko katika barua kumb. Na. LD/44/475/272/PJC ya tarehe 24 Januari 1972 kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo Mijini, aliyoandikiwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
 Kwa wakati huo, shughuli za ibada ya misa na mafundisho ya dini zilikuwa zikifanywa nje chini ya mkorosho kwenye ofisi ya Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge ambayo sasa ni ofisi ya CCM karibu na kituo cha mabasi ya Daladala Mwenge. Padre Adelhelm alisifu sana moyo wa Wakristo wa Mwenge. Yeye pamoja na Wakristo hao walikubaliana kujenga banda la ibada, na aliahidi kutoa mabati na misumari kwa ujenzi huo.
Tarehe 19 Januari 1974, Halmashauri iliandika barua kwa Katibu wa Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge, ikielezea nia ya Waamini kutaka kuanza ujenzi wa kibanda cha muda cha kusalia ndani ya eneo hilo, ambapo ma maombi hayo yalikubaliwa.

2.2 UJENZI WA KANISA LA MUDA
Hatua hii iliyofikiwa ilikuwa muhimu sana katika majadiliano na kuwavuta Wakristo wa Mwenge kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa kanisa. Ni kutokana na sababu hii hata Askofu Mkuu wa Jimbo aliandikiwa barua tarehe 24 Novemba 1973 akiombwa kibali na msaada wa kujenga kanisa, ukumbi wa Parokia na nyumba ya Mapadre. Uongozi wa Jimbo uliruhusu ijengwe “Parish Hall” kwanza, ambayo ingelitumika kama kanisa na kutoa angalizo kwamba ujenzi wa kanisa ungetegemea ongezeko la idadi ya Wakristo katika eneo la Mwenge.
Hatua muhimu na ya kimaendeleo iliyochukuliwa ilikuwa kujenga na kukamilisha kibanda cha kufanyia ibada Jumapili. Baada ya uongozi wa Kijiji kuridhia ombi la Wakristo kuanzisha kigango cha Mwenge, ujenzi wa banda la miti ulianza Januari 1974 kutokana na michango yao ya hiari. Kiasi cha shilingi 366/= kilipatikana na pia Padre Adelhelm alitoa msaada wa mabati, papi na misumari kama alivyoahidi. Banda hilo lililokuwa la miti na kukandikwa kwa udongo (matope) mwekundu lilikuwa na ukubwa wa meta 5 kwa meta 10. Hili ndilo lililokuwa kanisa la muda la kwanza la Mwenge ambalo lilikamilika mapema mwezi Aprili 1974. Hivyo, ibada za Juma Kuu zilifanyika ndani ya banda hilo na pia ibada ya Pasaka ikafanyika humo tarehe 14 Aprili 1974. Siku hiyo ya Pasaka ilikuwa ni sikukuu kubwa kwa Wakristo wa Mwenge kwani watoto 16 walipokea Komunyo ya Kwanza.

Hatua muhimu ya pili katika maendeleo ya Mwenge ilikuwa ni ujenzi wa ukumbi wa Parokia (Parish Hall) ambao baada ya kukamilika ulianza kutumiwa na kuendelea kutumika kama kanisa. Hatua hii ilizingatia ongezeko la Wakristo pamoja na juhudi zao na pia agizo la awali la Jimbo la kujengwa kwa Parish Hall. Ujenzi ulianza mwezi Mei 1974 na kukamilika Agosti 1974. Wafadhili wakuu wa ujenzi huo walikuwa Shirika la Mapadre wa Benediktini (Benedictine Fathers). Aidha, kwa msaada mkubwa wa Padre Adelhelm wa Parokia ya Mwananyamala, zilipatikana mbao za kukalia, meza, makabati na mapambo mengine ya ndani. Padre Adelhelm alisaidia pia kuwapatia wafadhili waliotoa kengele, kinanda na vifaa vingine vya ibada. Ujenzi wa ukumbi ulimalizika mwezi Agosti ambapo tarehe 15 Agosti 1974, ulifunguliwa rasmi ikiwa ni Sikukuu ya Kupalizwa Bikira Maria Mbinguni, Misa ya kwanza ilisomwa ndani ya ukumbi huu na Wakristo wakaanza kuutumia kwa ajili ya adhimisho la misa na ibada nyingine.

Baada ya kuhamia katika Parish Hall (wakati huo kanisa jipya), banda la miti lilitumika kama Shule ya Msingi ya Mwenge, baadaye banda hilo likaja kutumika kama Shule ya Chekechea (Kindergarten) pekee iliyokuwepo Mwenge kwa wakati huo. Katika kipindi cha mwaka 1975 hadi 1977, idadi ya Wakristo waliokuwa wanasali Mwenge ilizidi kuongezeka. Hii ilitokana na familia nyingi kuhamia katika nyumba zao katika maeneo ya Kitalu Na. 43 (Mwenge Kijijini), Vitalu Na. 44, 46 na 47 Kijitonyama. Ongezeko hili lilisababisha “kanisa jipya” kufurika Waamini hata ikabidi Paroko aongeze idadi ya misa za Dominika kufikia mbili. Pia aliamua kuwa, Padre kutoka Mwananyamala anayehusika na Mwenge, aitembelee mara tatu kwa wiki katika siku za kawaida ili kuwahudumia Wakristo.

3.0 MABADILIKO YA UONGOZI PAROKIA YA MWANANYAMALA
Mwaka 1978, palitokea mabadiliko katika uongozi wa Parokia Mama ya Mt. Martin De Porres, Mwananyamala. Mapadre wa Shirika la Mtakatifu Benedicto (OSB-Wabenediktini) baada ya kumaliza mkataba wao Desemba 1977, waliamua kwenda Kenya na nafasi yao kuchukuliwa na Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers). Chini ya uongozi wao, kulihimizwa kuongeza jitihada za kujitegemea kwa kuanzisha mfuko au akaunti maalumu ya Parokia na kufanya maamuzi ya kujiletea maendeleo. Kwa mfano ujenzi wa choo cha kudumu ulifanyika katika kipindi hiki na kusimamiwa na Halmashauri ya Kigango. Choo kilianza kutumika rasmi mwaka 1979.

Maendeleo ya kanisa la Mwenge yalizidi kushamiri. Eneo la kanisa lilizidi kupanuliwa na sehemu mpya ikaombwa kuongezwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Masista. Kibali kilitolewa na Chama cha Ushirika cha Ujenzi wa Nyumba Mwenge kwa barua Kumb. Na. RM/M/26/7/79 ya tarehe 26/7/1979.
Mwezi Julai 1979 yalitokea tena mabadiliko ya uongozi wa Parokia ya Mwananyamala, ambapo Mapadre wa Shirika la Wamisionari wa Afrika walipelekwa kufungua Parokia mpya ya Manzese na nafasi yao ilichukuliwa na Mapadre wa Shirika la Konsolata. Katika kipindi hicho, huduma za kiroho ziliendelea vizuri na idadi ya watoto waliopata Sakramenti ya Ubatizo, Ekaristi na Kipaimara iliongezeka mwaka hadi mwaka. Sakramenti ya Kipaimara iliendelea kutolewa Parokiani Mwananyamala hadi mwaka 1980.

4.0 KUTOLEWA SAKRAMENTI YA KIPAIMARA KIGANGONI MWENGE, 1981
Baada ya majadiliano ya muda mrefu baina ya Kigango cha Mwenge na Parokia Mama ya Mwananyamala kuhusu utolewaji wa Sakramenti ya Kipaimara ambayo muda wote ilikuwa inatolewa tu Mwananyamala, Mwenge iliomba watoto wa Mwenge wapewe Kipaimara palepale Mwenge na Askofu alikubali. Hivyo, Jumamosi tarehe 23 Mei 1981 Askofu alifika Mwenge kutoa Kipaimara jambo ambalo lilishuhudiwa na Waamini wengi pamoja na wageni mbalimbali. Ili kulipa Baraza la Kigango nguvu na madaraka zaidi katika kukabiliana na shughuli zake na kutaka lijitegemee hususan katika kuendeleza Kigango, baraza liliruhusiwa kuwa na mwakilishi Jimboni kuanzia mwezi Mei 1981.

5.0 KUPANULIWA KWA UKUMBI WA PAROKIA, 1982
Katika miaka ya 1980, Kigango cha Mwenge kilizidi kukua na mahitaji yake yakawa mengi zaidi. Hivyo Parish Hall ilipanuliwa mwaka 1982 na wakati huohuo ofisi ya Paroko na sakristia ziliongezwa kwa gharama ya shilingi 140,000/=. Mnara wa kengele pia ulijengwa na kukamilika. Kwa kazi hizi, kulibadili sura ya Parish Hall na kulifanya liwe na hadhi ya kanisa dogo.

5.1 UJENZI WA NYUMBA YA MAPADRE, 1983
Tarehe 24 Julai 1979, uongozi wa Kigango ulituma maombi Ushirika wa Mwenge ya kuongezewa eneo linalopakana na kiwanja cha kanisa kwa upande wa nyuma ya Parish Hall. Tarehe 26 Julai 1979, ombi hilo liliridhiwa na uongozi wa Chama cha Ushirika Mwenge. Ingawa barua ya maombi haikutaja matumizi ya sehemu hiyo, shabaha kubwa ilikuwa itumike kujenga nyumba ya Masista. Lakini awali ya yote katika kipindi cha mwaka 1980 – 81 mipango ya kujenga nyumba ya Mapadre ilianza kuandaliwa na Jimbo. Hii ilikuwa hatua ya mwanzo kwa Mwenge kuelekea kuwa Parokia. Katika miaka hiyo ilikadiriwa kuwa ujenzi wa nyumba ungegharimu shilingi 800,000/= au zaidi.

Kunako tarehe 2 Agosti 1981, Jimbo lilishapata shilingi 450,000/= na lilikuwa mbioni kupata kiasi kilichobaki ili ujenzi uanze. Aidha Baraza la Walei lilianza kuchangisha fedha kutoka kwa Waamini na Paroko wa Mwananyamala, Mhe. Padre Thomas alitoa nguo za mitumba za kuuza ili kupata fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi huo. Ilipofika tarehe 4 Oktoba 1981, Halmashauri ya Kigango ilielezwa kwamba Jimbo lilishafungua Akaunti kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mapadre ambayo ilikadiriwa kugharimu shilingi 1,000,000/=. Kutokana na makadirio hayo, Wakristo waliombwa kuchangia walau asilimia kumi (10%) ya kiasi hicho, sawa na shilingi 100,000/= ndani ya kipindi cha miezi sita.
Mwaka 1983 ujenzi wa nyumba ya Mapadre ulianza. Katika kipindi hiki kulikuwepo na changamoto kubwa ya kutokuwepo na usimamizi wa karibu na wa kutosha, na la pili na muhimu zaidi, ilikuwa bado kujulikana Shirika lipi litapewa jukumu la kuongoza Mwenge. Suala hili lilikuwa bado mikononi mwa Askofu Mkuu ambaye, alifanya juhudi kumpata Padre ambaye angeiongoza Parokia tarajiwa.

6.0 KUTEULIWA KWA SHIRIKA LA MUNGU MWOKOZI
Baada ya mawasiliano ya muda mrefu na Shirika la Wasalvatoriani, Mhe. Padre Zeno Zgudziak SDS aliteuliwa kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mapadre, hivyo akafika Mwenge kufanya kazi hiyo. Kuanzia mwezi Januari 1985 Padre Zeno Zgudziak SDS, alifanya kazi ya kusimamia ujenzi akisaidiawa na Baraza la Kigango pamoja na Wakristo. Alipewa msaada mkubwa na Waamini katika kukamilisha kazi ya ujenzi na mwezi Februari 1985, Padre Zeno aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Parokia tarajiwa ya Mwenge.
Mwezi Juni 1985, ujenzi wa nyumba ya Mapadre ulikamilika. Tarehe 16 Juni 1985 Mhe. Padre Zeno Zguadziak SDS aliteuliwa rasmi na kutangazwa kuwa Kigango cha Mwenge kimepata hadhi ya kuwa Parokia na kuwa yeye ndiye Paroko wa kwanza wa Parokia mpya ya Mwenge. Tarehe hiyohiyo, Padre Zeno alihamia kwenye nyumba ya Parokia, Mwenge.

6.1 KUJA KWA MASISTA WA SHIRIKA LA MISERIKORDIA (Masista wa Huruma)
Nyuma ya jengo  lililokuwa “Parish Hall” ambalo kwa muda mrefu (1974 – 1992) lilitumika kama kanisa na hivi sasa ni shule ya Chekechea, kuna majengo ya Shirika la Masista wa Misericordia wa Verona ambamo huishi Masista Wamisionari na Masista wazalendo wa Shirika hilo. Tangu kipindi cha miaka mingi Masista wa Shirika la Misericordia wa Tanzania walipenda kuishi katika jumuiya za Dar es Salaam kwa lengo la kueneza Karama ya Huruma. Pia katika kufundisha neno la Mungu na kushiriki katika shughuli zote za Parokia.

Mwaka 1979 Masista walitoa ombi kwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam Laurian Kardinali Rugambwa kuwapatia mahali pa kukaa, ambapo aliridhia waishi katika Parokia ya Mwenge.
Katika kipindi cha mwaka 1985, nyumba za kuishi Masista zilikuwa zikijengwa. Tarehe 17 Desemba 1986 Masista wawili, Sista. Luisacarla Rossi na Sr. N. Silvana Vettorello walihamia rasmi na kuanza maisha ya jumuiya. Baadae walijiunga Sr. Mary John na Sr. Agnes Matonya. Kuanzia mwaka 1987 walianza kufundisha dini mashuleni na kujihusisha na vyama vya kitume, hususan jumuiya ya Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) na pia kuanzisha Shirika la Watoto la Kipapa (VIPAPA). Kuwepo kwa Masista hawa kuliongeza ubora wa kazi za kitume, kwani manufaa mengi yalipatikana kutokana na kuwafundisha wasichana na akina mama hasa kazi za kushona na kazi nyingine za mikono zikiwemo za mapishi. Pamoja na kazi hizo, Masista hawa hushughulika na kazi za kanisa kama vile mafundisho ya watoto wa Komunio ya Kwanza, Kipaimara na kufundisha somo la dini katika shule za msingi ndani ya Parokia.

Aidha, kwa miaka ya hivi karibuni, mapema mwaka 1996, baada ya kupewa jengo la Ukumbi wa Parokia (kanisa la zamani) walilifanyia ukarabati mkubwa kwa madhumuni ya kujenga kituo cha watoto wadogo na kuanzisha shule ya chekechea kwa watoto wenye umri wa miaka 4 hadi 6. Shule hiyo ya chekechea inajulikana kama Bikira Maria Nyota ya Bahari. Mkataba kuhusu ujenzi na uendeshaji wa kituo hicho katika Parokia ya Mwenge uliridhiwa tarehe 5 Septemba 1996 na Askofu Mkuu Mhashamu Polycarp Kardinali Pengo, Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Mama Mkuu wa Masista wa Misericodia, Kanda ya Tanzania.

7.0 UZINDUZI WA PAROKIA YA MT. MAXIMILIAN MARIA KOLBE, MWENGE
Tarehe 29 Septemba 1985, Parokia ya Mwenge ilizinduliwa rasmi na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa aliyekuwa askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam. Misa ya uzinduzi ilihudhuriwa na maelfu ya Wakristu waliokadiriwa kufikia 1,500 wakiwemo viongozi wa serikali.
Kwa namna Fulani kati ya Vigango vya Jimbo Kuu la Dar es Salaam vilivyobahatika kupandishwa hadhi, Mwenge ilishika nafasi ya pekee. Kwanza maendeleo yalikuwa ya haraka. Pili Wakristo walikuwa na ari kubwa sana kiasi wakati mwingine Jimbo liliona kama vile linasukumwa. Lakini jimbo pia liliitikia, kwani Mwenge ilipewa hadhi ya Parokia hata kabla ya kutangazwa rasmi na Askofu Mkuu.  Hii ilitokana haswa na ushirikiano kati ya Baraza, Wakristu na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mwananyamala Padre Aloisi Accossato I.M.C. ambaye kwa namna ya pekee alivutiwa sana na taratibu za Mwenge na daima aliunga mkono maamuzi ya Baraza la Kigango. Mwenge hata hivyo sio wakati wote walionekana kuwa wazuri ila wakati fulani wajumbe wa Baraza la Mwenge waliitwa wakorofi kwa ile ari yao ya kutaka uamuzi fulani ufanyike haraka na mara nyingine bila kusubiri maoni ya Baraza la Parokia Mama.

Wakati Mwenge inazinduliwa kuwa Parokia mwaka 1985, ilikisiwa kuwa na Waamini wapatao 10,000 au zaidi wakiwa wanaishi katika maeneo yafuatayo: Kijitonyama yenye Mwenge Kijijini (Kitalu Na. 43); Vitalu Na. 44, 46 na 47; Mwenge Jeshini, Mlalakuwa na Mikocheni. Maeneo matano ya Sinza (Vitalu A mpaka E) ambayo sasa ni Parokia; na eneo la Makumbusho Kijijini na Makumbusho Flats yaliongezwa baadae. Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka 1994, inayozingatia kuongezwa kwa maeneo hayo mawili hapo juu, idadi ya Waamini iliripotiwa kufikia 10,500. Tangu kuzinduliwa kwake, Parokia iliendelea kustawi na idadi ya Waamini kuongezeka hadi Vigango vyake vya Sinza na Mikocheni navyo vikakua na kupata hadhi ya Parokia mwaka 1997 Sinza na 2006 Mikocheni.

7.1 MWENGE PAROKIA CHANGA: 1985 – 1997
Katika awamu ya miaka hii (1985 – 1997), Parokia ya Mwenge ilistawi kiuchungaji na ikafanikiwa kupata vigango viwili. Kigango cha Sinza kilichokabidhiwa rasmi kwa Parokia ya Mwenge  tarehe 23 Oktoba 1985, kiliendelezwa na hatimaye mwezi Desemba 1997 kikapata hadhi ya kuwa Parokia, na cha pili ni Kigango cha Mikocheni. Aidha, mafanikio hayo yaliweza kupatikana pamoja na mambo mengine ya kuonyesha jinsi Parokia ilivyoshika kasi kubwa ya maendeleo katika kipindi hicho, yakiwemo yafuatayo:

•    Kujenga Kanisa jipya Mwenge ambalo lilibarikiwa tarehe 16 Agosti 1992;
•    Kujenga Kanisa la Kigango cha Sinza lililozinduliwa rasmi tarehe 30 Aprili 1989;
•    Kujenga nyumba ya Mapadre  wa Mwenge na Sinza zenye gorofa moja;
•    Kuanzisha na kuendeleza Kigango cha Mikocheni;
•    Kupadrishwa kwa Shemasi Henry Mchamungu tarehe 24 Juni 1994 akiwa tunda la kwanza la Parokia ya Mwenge;
•    Kupadrishwa kwa Shemasi Paul Njoka tarehe 5 Julai 1997 akiwa tunda la pili la Parokia;
•    Upanuzi wa kiwanja cha Mwenge kwa kununua nyumba Na. 382/43, Agosti 1997;
•    Ujensi wa Grotto la kwanza la Bikira Maria, ukingoni mwa Maximilian Square Mwenge;
•    Uinjilishaji kupitia Kwaya ya Mt. Cesilia Mwenge hasa kwa kanda za Mwaka wa Bikira Maria (1987-1988) na ujio wa Baba Mtakatifu mwaka 1990 nk

8.0 UJENZI WA KANISA LA KUDUMU, MWENGE
Haja ya kuwa na kanisa kubwa Mwenge, ilikuwa imeanza kuonekana hasa wakati Jimbo lilipoamua kukifanya Kigango cha Mwenge kuwa Parokia kwa vile idadi ya Wakristu ilikuwa inaongezeka kwa sababu watu walikuwa wanahamia maeneo mapya ya Kijitonyama. Hivyo, katika kuipa Mwenge hadhi ya Parokia ilibidi mipaka yake ya kuhudumia ipanuliwe kiparokia kwa kuongeza eneo lote la Sinza (ambalo robo tatu yake lilikuwa chini ya Parokia ya Manzese – Kanda ya Sinza), eneo la Mikocheni B (ambalo lilikuwa nusu yake linahudumiwa na Parokia ya Kawe na nusu nyingine ikihudumiwa na Parokia ya Mt. Petro Oysterbay).

Mahitaji ya Kanisa jipya yalijionyesha wazi pia kanisani Mwenge katika idadi kubwa ya Waamini waliokuwa wanahudhuria misa siku za Dominika mwezi Novemba 1985, Mwezi Januari 1986 ilibidi ianzishwe misa ya nne ili kupunguza msongamano katika misa zilizokuwepo. Wakati huohuo, Paroko alilazimika kuanzisha Kigango kuhudumia Wakristo waliokuwa wanakaa eneo la Sinza, pamoja na kwamba viongozi wa Jimbo walikuwa wamemtahadharisha Paroko kuhusu upatikanaji wa Mapadre wa kuja Mwenge kumsaidia katika kutoa huduma za kichungaji. Kuanzishwa kwa Kigango Sinza kulipunguza kwa kiasi kikubwa msongamano kwenye misa katika kikanisa cha Mwenge. Hata hivyo msongamano ulizidi kuongezeka na ufumbuzi wake haukuonekana dhahiri.

Mwezi Juni 1986 Baraza la Walei la Parokia lilipitisha azimio la kuanzisha mchango wa kudumu ili kuwe na mfuko wa kujenga kanisa jipya. Mchango huu ulizinduliwa rasmi tarehe 17 Agosti 1986.
Wakristo wa maeneo yote walifahamishwa uamuzi huu na mikakati ya kuwashirikisha katika ujenzi wa kanisa jipya ulianzishwa rasmi kwa kuwachangisha kila familia katika maeneo yao wanakoishi. Michoro ya Ramani ya kanisa jipya la Mwenge ilianza kutayarishwa mapema na misaada ya fedha ilianza kutafutwa kutoka kwa wafadhili mbalimbali ndani na nje ya nchi. Wa kwanza kupelekewa ombi la msaada na ambao walikuwa wa kwanza kuitikia, walikuwa ni uongozi wa Shirika la Wasalvatoriani ambao walitembelea Parokia ya Mwenge na kujumuika na Waamini katika misa walioiadhimisha tarehe 29 Juni, 1986. Aliyekuwa Balozi wa Papa hapa Tanzania wakati huo, Askofu Mkuu Vicenso Moreni alikuwa wa kwanza kuombwa msaada wake wa hali na mali. Msaada wa Balozi ulitolewa kwa njia ya ushauri wa aina ya kanisa ambalo linafaa kwa hapa Mwenge na pia msaada wa fedha uliotolewa na Ofisi ya “Propaganda Fide” huko Roma. Wafadhili wengine walioombwa msaada walikuwa ni Shirika la “Missio” la Ujerumani Magh’aribi na Mashariki na mashirika mengine ya kidini ya huko Ulaya na Amerika. Kutokana na michango ya Wakristu pamoja na michango ya wafadhili kutoka nje ya nchi, fedha iliyopatikana iliwezesha kuanza ujenzi katua ya kwanza. Ujenzi ulianza rasmi Oktoba 1988 kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni kujenga nguzo na paa, kazi ambayo ilipewa Kampuni ya “Italfrem”. Ujenzi uliendelea vizuri, na ilipofika mwisho wa mwaka 1988 nguzo zote na kenchi pamoja na mashimo ya kusimamisha nguzo vilikuwa tayari vimemiminwa.

Baada ya hatua ya kwanza kukamilika, ujenzi uliingia awamu ya pili, kazi iliyopewa Kampuni ya “J.W. Ladwa”. Ujenzi uliendelea vizuri, na michango ikawa inaendelea, kwa kubuni mbinu mbalimbali za kupata fedha, ikiwa ni pamoja na kuandaa Matembezi ya Hiari (Charity Walk), mnada wa vitu mbalimbali nk. Ilipofikia mwezi wa Oktoba 1991 Kanisa likawa limekamilika.
Kanisa jipya lilizinduliwa rasmi na kubarikiwa mwaka 1992 na Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Uzinduzi ulifanyika sanjari na kusherehekea Sikukuu ya Somo wa Parokia Mt. Maximilian Kolbe. Miongoni mwa wageni mashuhuri waliohudhuria sherehe hiyo, ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Samweli Malechela (MB) akiwakilisha serikali, wageni kutoka Parokia mbalimbali, viongozi na wageni wa madhehebu ya kiroho

9.0 VIGANGO VYA PAROKIA YA MWENGE
9.1 Kigango cha Sinza
Juhudi za kuanzisha kigango Sinza zilianza mnamo mwaka 1981. Mwanzoni Wakristo wa Sinza walikuwa wakisali kwenye makanisa ya Manzese, Chuo Kikuu na hata Kanisa la Mt. Yosef. Wakati huo, Parokia ya Manzese, chini ya uongozi wa Paroko, Padre Geraldo Chebanon ilikuwa ikimiliki Kanda zake za Tandale Makuburi, Sinza, Ubungo National Housing nk. Ibada ya kwanza katika eneo la Sinza ilifanyika mwaka 1981 kwenye shule ya msingi Mugabe. Baada ya misa kulikuwa na kikao cha wakristo wa maeneo ya Sinza ambao waliona umuhimu wa kuwa na kanisa katika eneo hilo. Kuanzia tarehe 3 Aprili 1982, hoja ya kiwanja cha kanisa Sinza ilijitokeza. Ilipofika Oktoba 1983 mikakati ya ujenzi wa kanisa ilianza na jiwe la msingi kuwekwa mwaka 1984. Wakati huo, bado uamuzi wa Parokia ipi itakuwa msimamizi wa Kanisa la Sinza, kati ya Manzese na Mwenge haikuwa imejulikana hadi tarehe 30 Septemba 1985, siku moja tu baada ya Mwenge kuzinduliwa kuwa Parokia, ndio Waamini wa Sinza wakatangaziwa kuwa Sinza itakuwa chini ya Parokia mpya ya Mwenge.
9.2 Kigango cha Mikocheni
Eneo la Mikocheni lilionekana zaidi baada ya Mwenge kuwa Parokia mwaka 1985. Watu wa eneo hili walikuwa wanasali Parokia za Kawe, Mt. Petro Oysterbay, Upanga na Mt. Yosef. Uongozi wa Jimbo uliamua eneo la Mikocheni liwe chini ya Parokia ya Mwenge na hadi kufikia tarehe 30 Mei 1998 idadi ya Waamini katika Kigango hicho cha Mt. Martha Mikocheni ilizidi kuongezeka. Harakati za kutafuta kiwanja cha kujenga zilianza kwa kasi, na Hati Na. 47558 ya Kiwanja iliyotolewa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi cha tarehe 26 Julai 1998 ilikabidhiwa uongozi wa Kigango. 
Baada ya kupata hati hiyo, kanisa la muda lilianza kujengwa na huduma ya misa kutolewa kuanzia tarehe 25 Aprili 1999. Juhudi za kukiendeleza Kigango hicho ziliendelea na ujenzi wa Kanisa la kudumu ulianza tarehe 29 Julai 2002 na tarehe 26 Oktoba 2002 jiwe la msingi liliwekwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Hatua kwa hatua, Ujenzi wa Ofisi (2003) na nyumba ya Mapadre (2005) ulifanyika, na baada ya kukamilisha shughuli zote ilipofika tarehe 24 Juni 2006 siku ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa watoto wa Kigango cha Mikocheni, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, wakati      

10.0 UNUNUZI WA NYUMBA YA WAGENI, MWENGE
Mwezi Agosti 1997, Parokia ilinunua nyumba Na. 382/43 ambayo inapakana na kiwanja cha kanisa. Lengo la kununua nyumba hiyo, ilikuwa kupanua eneo la kanisa ili kupata nafasi ya kutosha kuegesha magari ya waamini na pia nafasi ya michezo na burudani kwa vijana. Nyumba hiyo ilinunuliwa kwa mkopo wa shilingi 15,000,000/= ambazo waamini walichangia urejeshwaji wake. Mwaka 2004 nyumba hiyo ilifanyiwa ukarabati mkubwa na ikaanza kutumika kama nyumba ya wageni wa Parokia, hususan Mapadre, Mabruda, Mafrateri nk. Kuanzia Mwezi Mei 2008, nyumba hiyo ilianza kutumiwa na Mapadre wakazi kutokana na kuvunjwa kwa nyumba ya zamani.

10.1 UJENZI WA GROTTO JIPYA LA BIKIRA MARIA
Wazo la kujenga Grotto la Bikira Maria lilijitokeza na mwaka 2005 ujenzi ulianza rasmi na kukamilika 2006. Liliwekewa sanamu ya Bikira Maria, iliyotolewa zawadi na Masista wa Misericordia. Grotto hilo lilizinduliwa na kubarikiwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo tarehe 10 Novemba 2007.

10.2 UTAFUTAJI NA UNUNUZI WA KIWANJA/ENEO MLALAKUWA
Baada ya Kigango cha Mikocheni kupata hadhi ya Kigango tarehe 26 Novemba 2000, uongozi wa Parokia ya Mwenge ulijielekeza kwenye hoja iliyokuwa imekaa kiporo kwa miaka mitatu tangu mwaka 1997. Wakati huo, pendekezo lilitolewa na kukubaliwa na kikao cha Halmashauri Walei kwamba, Kanda ya Mlalakuwa iandaliwe kuwa Kigango. Ili kufanikisha azma hiyo, Kamati Tendaji ilikuwa imehimiza kwamba Waamini wa Kanda hiyo watafute sehemu maalum ya kufanyia ibada kwenye eneo hilo. Hata hivyo juhudi hizi hazikuzaa matunda. Suala hili lilisuasua na hata kusahaulika hadi mwaka 2003 lilipoibuka tena kwa taarifa iliyoletwa na uongozi wa Mlalakuwa kuwa eneo la takriban robo tatu za ekari limepatikana na linauzwa kwa kiasi cha shilingi 45,000,000/=. Uongozi wa Parokia ulienda kulikagua, na kuridhia kuwa ni eneo zuri kwahali ya Mlalakuwa. Kiasi kilichotajwa kilionekana kuwa changamoto kubwa kwa vile Parokia ilikuwa na miradi miwili ya kujenga kwa wakati mmoja, kanisa na nyumba ya Mapadre Mikocheni iliyokuwa inaendelea kwa nguvu za waamini wa Parokia ya Mwenge.
Tarehe 10 Desemba 2003, uongozi ulifanya mawasiliano na uongozi wa Jimbo kuomba msaada wa fedha na mkopo wenye masharti nafuu kwa ajili ya kufanikisha ununuzi wa kiwanja hicho. Tarehe 29 Desemba 2003 na 6 Januari 2004 viongozi wa Jimbo walifika Mwenge na kujionea eneo hilo na kuafiki linunuliwe. Katika mazungumzo yaliyofuata, Jimbo lilikubali kutoa mkopo wa shilingi 20,000,000/= ili mradi fedha hiyo irudishwe kabla ya tarehe 30 Aprili 2005 na wakati huohuo ziongezwe jitihada za kutafuta tofauti iliyobaki ya shilingi 25,000,000/= kukamilisha  jumla ya shilingi 45,000,000/= zilizohitajika na muuzaji. Kwa kuzingatia majukumu yaliyokuwepo, pamoja na Jimbo kujitolea kiwango hicho,bado waamini wa Mwenge hawangaliweza, na hivyo kulazimika kuahirisha zoezi hilo hadi hapo majukumu ya Mikocheni yatakapomalizika.
Katika kikao cha Halmashauri Walei kilichofanyika tarehe 6 Aprili 2008 ilitolewa taarifa kuwa kiasi cha shilingi 2,000,000/= ndizo zilikuwa zimekusanywa. Aidha, gharama za viwanja ziliendelea kupanda  hadi eneo husika kufikia shilingi 300,000,000/- mwaka 2009.

10.3 UJENZI WA NYUMBA MPYA YA MAPADRE:
Kazi ya ujenzi wa nyumba mpya ya Mapadre ilianza kwa kufanya maandalizi ya awali kwa kupata michoro inayokidhi, pamoja na kibali cha ujenzi Na. 004947 kilichotolewa tarehe 10 Desemba 2007. Wakati huo waamini walianza kuchangia juhudi za ujenzi. Tarehe 12 Agosti 2007, wafadhili wa ndani walikutana na kuanzisha rasmi mfuko wa ujenzi kwa kufanya uchangiaji (Fund Raising) uliofana kwa kiasi kikubwa. Kutokana na juhudi hizo hadi kufika Aprili 2008, kiasi cha 30,000,000 taslimu zilikuwa zimeshapatikana. Ujenzi ulianza rasmi tarehe 1 Mei 2008 kwa kumkabidhi  mkandarasi M/S Eagle Building Contractors ambaye alifanya kazi hiyo chini ya usimamizi wa kamati teule. Katka kutekeleza mradi huu, jengo la zamani lilivunjwa ili kupisha ujenzi wa nyumba mpya. Mkandarasi alianza kuvunja nyumba ya zamani kati ya tarehe 2 na 24 Mei 2008. Kazi ya kuchimba msingi ilianza rasmi 2 Juni 2008, na kumalizika tarehe 12 Juni 2008. Hadi kufikia tarehe 31 Agosti 2009  ilikuwa imekamilika tayari kwa Mapadre kuhamia. Nyumba ilibarikiwa na kuzinduliwa rasmi tarehe 6 Septemba 2009 na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Uzinduzi wa nyumba ulitanguliwa na n ibada maalumu ya misa ya shukrani iliyoongozwa na Mwadhama, ambapo pia alibariki kengele ya umeme inayogonga kwa kutumia mtambo wa kisasa (automatic).

10. 4 KUSIMIKA SANAMU YA MT. MAXIMILIAN MARIA KOLBE.
Suala la kupata na kusimika sanamu lilianza kwa juhudi zilizofanywa na Paroko, Padre Christopher Luoga, SDS pamoja na Paroko Msaidizi Padre  Stanslaus Goral SDS, kwa msaada wa Mkuu wa Shirika la Wafransiskani wa Conventuale, walioko Parokia ya Segerea. Kwa ujumla wake, Gharama ya ununuzi, usafirishaji, kodi ya forodha na gharama nyingine kutoka Poland hadi Dar es Salaam ilikuwa dola za Kimarekani 3,150 (USD 3,150). Sanamu hiyo iliwasili Mwenge tarehe 27 Juni 2009 na kazi ya kuijengea ikaanza, na hadi ilipokamilika, uzinduzi ulifanyika tarehe 20 Agosti 2009 kwa Ibada ya iliongozwa na Mhashamu Methodius Kilaini, Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Katika ibada hiyo ya kusimika sanamu ya Mt. Maximilian Maria Kolbe lilifanyika pia tukio jingine la kubariki msalaba maalumu wa Jubilei ya Fedha ambao ulianza kuzungushwa na waamini katika JNNK kikanda.

11.0 WATAWA WALIOONGOZA NA KUFANYA KAZI ZA KITUME MWENGE: 1985 - 2018
11.1 Maparoko na Maparoko Wasaidizi
Kama ilivyodokezwa awali Parokia ya Mwenge ilianza Septemba 1985. Katika kipindi chote hiki imekuwa ikiongozwa na kuhudumiwa na Mapadre Wamisionari wa Shirika la Mungu Mwokozi (Wasalvatoriani) chini ya Maparoko wa kudumu kwa vipindi mbalimbali na kwa mpangilio ufuatao:



MWAKA
JINA LA PAROKO
MPANGILIO
PAROKO MSAIDIZI
MWAKA
1
Feb 1985 – Okt 1986
Padre Zeno Zgudziak, SDS
Paroko wa Kwanza

Pd. Andrea Kielkowski, SDS
Pad. Mathias Millanzi, SDS

Jan 1986 – Jun 1986
Ago 1986 - Jan 1988

Ago 1985 – Des 1985
Pd. Andrea Mysiura, SDS
Paroko wa Muda
Pd. Carol Gleason, SDS
Des 1988 – 1991
2
Jun 1986 – Sep 1991
Padre Karol Szojda, SDS
Paroko wa Pili
Pd. Mathias Millanzi, SDS
Jan 1992 - Des1992
3
Jan1993 – Mei 1994
Pd. Mathias Millanzi, SDS
Paroko wa Tatu
Pd. Engelbert Hatlapa, SDS
1991 - Ago 1993
4
Ago1993 – Nov 1995
Pd. James Aloys Weyker, SDS
Paroko wa Nne
Pd. Carol Gleason, SDS
Mei 1993 – 1995
5
Nov1995 – Feb 1996
Pd. Mieczyslaw Kijaczek, SDS
Paroko wa Tano


6
1996 – 1998
Pd. Krystian Golisz, SDS
Paroko wa Sita
Pd. Christopher Luoga, SDS
Pd. Felix Kisaka, SDS
Pd. Jude Massawe, SDS
Ago 1997 - 1998
Ago 1998

Juni 1998 – 1999

7
1999 – 2002
Pd. Jude Massawe, SDS
Paroko wa Saba
Pd. Marian Hajzyk, SDS
Ago 2000 – Des 2001
8
2002 - Nov 2011
Pd. Christopher Luoga, SDS
Paroko wa Nane
Pd. Stanslaus Goral, SDS
2002 –
9
Jan 2012 – Ago 2012
Pd. Vilanova Mahoo, SDS
Paroko wa Tisa
Pd Amon K.  Swai, SDS
Pd.AusonKamughisha, SDS
Pd. Baraka Isuja, SDS
2005 - 2006
2006 - Feb2008
Ago 2008 – Okt 2008
10
Ago 2012 – Feb 2013
Pd. Vincent Sabiiti, SDS
Paroko wa Kumi


11
Mar 2013 -
Eugine Reslinski
Paroko wa 11
Pd. Sixbert Heri, SDS
Pd. Felix Mkude, SDS
Pd. Jeremia Msaki, SDS
2013
2015
May 2018

11.2 WATAWA
Pamoja na Paroko akiwa na wasaidizi wake, pia kumekuwepo na Watawa wa kike na wa kiume kwa maana ya Masista na Mabruda ambao wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali ndani ya Parokia kama vile Katekesina kulea Vyama vya Kitume nk. Hao ni pamoja na Mabruda wa Salvatoriani na Masista wa mashirika yafuatayo:

•    Masista wa Misericordia wa Verona (I.S.M.)
•    Masista wa Shirika la Bibi Yetu wa Kilimanjaro (C.D.N.K.)
•    Masista wa Shirika la Mt. Theresia (C.S.T.)
•    Masista wa Shirika la Moyo Safiwa Maria, Mgolole Morogoro (C.I.M.C.)
•    Shirika la Mabinti wa Maria (Daughters of Mary Immaculate-D.M.I.) Tabora
•    Masista wa Shirika la Salvatoriani (SDS)

11.2.1 Masista wa Misericordia wa Verona (I.S.M.)
Masista wa wa Shirika la Misericordia ndio waliokuwa wa kwanza kufanya kazi katika Parokia ya Mwenge. Hili ni shirika la kimisionari la kimataifa lenye makao yake makuu kule Verona nchini Italia. Kwa hapa Tanzania makaoyake makuu yapo Dodoma. Sr. Luisacarla Rossi pamoja na Sr. N. Silivana Vettorello ndio waliofika kwanza Parokiani tarehe 17 Desemba 1986. Baadaye walikuja masista wawili kujiunga nao; Sr.Mary John na Sr. Agnes Matonya. Tangu wakati huo Masista wa Shirika hili wameendelea kufanya kazi mbalimbali hapa Parokiani hadi hivi sasa. Hufundisha somo la dini shule za msingi, hutoa mafundisho kwa watoto wanaojiandaa kupokea Komunio ya Kwanza na Kipaimara, hulea vyama vya kitume vya WAWATA, VIWAWA na VIPAPA, hushughulika na usafi na upambaji wa kanisa na pia huendesha  shule yao ya elimu ya awali ya Bikira Maria Nyota ya Baharii iliyopo hapa Parokiani Mwenge.

11.2.2 Masista wa Shirika la Bibi Yetu wa Kilimanjaro (C.D.N.K.)
Masista wa Shirika la Bibi Yetu wa Kilimanjaro (C.D.N.K.), walifika Mwenge mwanzoni mwa mwaka 1993 na kununua nyumba Na. 375/43 katika eneo laMwenge jirani sana na eneo la kanisa. Masista waanzilishi walioanza katika nyumba hiyo ni Sr. Oresta Uisso, Sr. Agricolla Soka na Sr. Innocensia. Mara tu walipofika walishiriki kwenye kazi za Parokia za uinjilishaji ikiwemo ihamasishaji uanzishaji wa Legio Maria. Mwaka 1994, Masista hawa walianza pia kufundisha somo la dini katika shule za msingipamoja na kutoa mafundisho kwa watoto wanaojiandaa kupata Komunio ya Kwanza na Kipaimara. Mpakasasa, Masista hawa bado wanaendelea na kazi yao ya uinjilishaji pamoja na kusaidia kazi za liturjia na ibada mbalimbali kanisani.

11.2.3 Masista wa Shirika la Mt. Theresia (C.S.T.)
Masista wa Shirika hili ambao makao yao makuu yako Iringa ni kutoka shirika la wamissionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu (Teresia Mdogo) Wateresina au Congregation Saint Teresia (CST), walifikaMwenge tangu mwaka 1997. Mwezi Julai 2003 walihamia na kuanza kuishi katika nyumba yao iliyoko Mikocheni A. Tangu wakati huo wamekuwa wakishughulika na kazi za utume na umissionarikwa njia mbalimbali kama vile kufundisha dini,uuguzi, ukatekista na maendeleo ya jamii (umaritane). Kabla ya Kigango cha Mikocheni kuwa na ukumbi, Masista wa shirika hili la Wateresina walikusanya watoto nyumbani na kuwafundishasala, michezo na nyimbo Sunday School). Baadaye Parokia ya Mwenge iliwaomba rasmi wafanye kazi yakufundisha vipindi vya somo la dini shuleni na Katekisimu kwa watoto wa mafundisho ya Komunio ya Kwanza na kipaimara kwa Kigango cha Mikocheni. Baada ya Mikochenikuwa Parokia, Masista hawa wameendelea kutoa huduma katika Parokia ya Mt. Martha Mikochenina Mt. Maximilian Kolbe Mwengechini ya usimamizi wa Mama Mkuu Sr. Florence Lutambi.

11.2.4 Masista wa Shirika la Moyo Safi wa Maria, Mgolole Morogoro (C.I.M.C.)
Masista wa shirika hili walifika Mwenge tarehe 10 Januari 2003 wakiwa na lengo kuu la kufanya kazi za utume ambazo ni kufundisha dini, kulea watoto yatima, kusaidia wagonjwa,kutengeneza vifaa mbalimbali vya kanisa na kufanya kazi za kichungaji kadiri ya mwongozo wa jimbo.

11.2.5 Masista wa Shirika la Mabinti wa Maria (Daughters of Mary Immaculate-D.M.I.) Tabora
Shirika la Mabinti wa Maria wa Tabora (Daughters of Mary Immaculate – D.M.I.) ni shirika lakitawa la kijimbolenye makao yake makuu Jimbo Katoliki la Tabora. Mwanzoni kabisa Masista hawa, walifika Mwenge kutoa huduma wakitokeakwenye nyumba yao iliyopo Msimbazi. Mwishoni mwa mwaka 1993walinunua nyumba huko Sinza Kitalu A ambapo masista wawili: Sr. Maria Stella Mlangalla na Sr. Ana Mwacha walianza kuishi nakushiriki kwenyekazi mbalmbal.Hatimaye mwaka 1995 Masistahawa walihamia kwenye nyumba yao eneo la Sinza (Barabara ya Sam Nujoma) ambapo pia wamejenga hospitali na shule ya chekechea. Chanzo cha kufika Parokia ya Mwenge wakati huo, na sasa Parokia ya Sinza ni kutoa utume kwa jamii, hususan kufundisha elimu dunia shule za msingi na dini shuleni.Wakati Sinza ikiwa bado ni kigango chini ya Mwenge, Masista hawa walitoa huduma katika maeneo ya kigango na tangu mwaka 1998 baada ya Sinza kuwa Parokia, Masista hawa wameendelea kutoa huduma ya kufundisha shule za msingi pamoja na kufundisha somo ladini katika shule zilizokondani ya Parokia hiyo.

11.2.6 Masista wa Shirika la Salvatoriani (SDS)
Hawa walifanya kazi kuanzia tarehe 26 Septemba 2003 hadi 2005. Waliombwa kusaidia kufundisha dinikutokana na uhaba wa kuwapata walimu wa dini. Ni Sr. Mechtides Nambunga SDS ndiye aliyeziba pengo la uhaba wa Makatekista.

12.0 VIONGOZI HALMASHAURI WALEI
Kwa kuzingatia kwamba uongozi ndani ya Parokia unajumuisha pia viongozi wa Halmashauri Walei, ni vema kuitazama historia ya uongozi kadiri ilivyobadilika katika vipindi mbalimbali vya uongozi. Kadiri ya Katiba ya Halmashauri ya Walei Katoliki Tanzania (2001, 2003), uongozi ndani ya Parokia huzingatia kuwepo kwa Halmashauri Walei Parokia na Kamati Tendaji ya Parokia. Uongozi wa Halmashauri ulikuwa na utaratibu wa kuwa na viongozi watano (5) wa Kamati Tendaji wa kuchaguliwa na Halmashauri ya Parokia yenye wajumbe watatu (3) wa kuteuliwa na Paroko.
Katika kipindi cha 1985 – 2010, uongozi wa Parokia uliimarishwa kwa kuwashirikisha viongozi Halmashari Walei walioshika nyadhifa mbalimbali kwa mujibu wa katiba na kuunda Kamati Tendaji za Parokia kwa vipindi mbalimbali vinavyoonyeshwa. Muundo wa sasa wa Halmashauri Walei unaundwa na viongozi watano (5) wa Kanda na Kamati Tendaji ya Parokia, ambao ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina na Wenyeviti wa Vyama vya Kitume ngazi ya Parokia.

KAMATI TENDAJI YA HALMASHAURI WALEI KUANZIA MWAKA 1985 - 2018



MWAKA
KIONGOZI
WADHIFA
1
1985 –1986
Helena Khamsini
Peter Masaiya

Simon Mnimbo
Theodore Mahulu
Athanasi Mapunda
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina

1986 –1987
Peter Masaiya
Nathalia Mlengule
Theodore Mahulu
Elly Iwato
Atanas Mapunda
Joseph Dalotta
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
Mweka Hazina Msaidizi
2
1988 –1990
Peter Masaiya
Nathalia Mlengule
Theodore Mahulu
Elly Iwato
Atanas Mapunda
Joseph Dalotta
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
3
1991 –1993
Peter Masaiya
Gosbert Mbatina
Theodore Mahulu
Elly Iwato
Atanas Mapunda
Joseph Dalotta
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
4
1993 – 1995
Peter Masaiya
Gosbert Mbatina
Theodore Mahulu
Elly Iwato
Atanas Mapunda
Joseph Dalotta
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
Mweka Hazina Msaidizi
5
1995 – 1997
Gosbert Mbatina (RIP)
Daniel M. Ndabi
Edgar Kivenule (RIP)
Juliana Mbogautwa
Thomas Kadushi
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
6
1997 – 2001
Helena Khamsini
Daniel M. Ndabi
Lazaro Mwakimbala
Elly Iwato
Justine Uiso
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
7
2001– 2003
Daniel M. Ndabi
Athanas Mapunda
Severin Mbuya (RIP)
Thomas Kadushi
Joseph Mushumbusi
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
8
2004- 2006
Athanas Mapunda
Daniel Ndabi
Severin Mbuya (RIP)
Prosper Vedasto/Maria Mboye
Joseph Mushumbusi
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
9
2007 – 2009
Peter M. Ngowi
Theresia Nzunda
Maria Mwaka Mboye
Solanus Ndunguru/Susan Mugurusi
Aloisi Mwanga/Batilda Mnzava
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
10
2010 – 2013
Peter M. Ngowi
Solanus Ndunguru
Maria Mwaka Mboye
Prosper Vedasto
Batilda Mnzava
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
11
2013 - 2015
Linus A. Ngowi
Anatoli Paulo
Susan Mugurusi
Francis Moshi
Batilda Mnzava
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina
12
2015 -
Linus A. Ngowi
Anatoli Paulo
Susan Mugurusi
Francis Moshi
Batilda Mnzava
Mwenyekiti
Makamu Mwenyekiti
Katibu
Katibu Msaidizi
Mweka Hazina

12.1 KAMATI ZA PAROKIA
Parokiani kuna Kamati Ndogondogo tano (5) za Kikatiba ambazo zinasimamia masuala mbalimbali ya Parokia. Wenyeviti wa Kamati hizo, ni wajumbe wa Kamati Tendaji ya Parokia. Kamati hizo ni:


KAMATIMWENYEKITI
1
Malezi na FamiliaMwenyekiti;            Kamati Tendaji
2
Ibada na LiturjiaMakamu M/Kiti;     Kamati Tendaji
3
Haki na AmaniKatibu;                     Kamati Tendaji
4
Elimu, Mafundisho ya Dini na TeolojiaKatibu Msaidizi;      Kamati Tendaji
5
Mipango, Uchumi na FedhaMweka Hazina;       Kamati Tendaji

Aidha, pamoja na Kamati hizo, kuna Kamati nyingine ndogondogo vilevile ambazo siyo za kikatiba ambazo zimeundwa katika Parokia, ambazo ni:

  • Kamati ya Ulinzi
  • Kamati ya Afya
  • Kamati ya Ardhi

12.2 UONGOZI WA KANDA
Viongozi wa Kandani wajumbe wa Halmashauri Walei Parokia. Hadi mwaka 2000, kila kanda ilikuwa inawakilishwa na Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti naKatibu. Kuanzia mwaka 2001 uwakilishi katika Halmashauri uliongezeka kwa kuongeza nafasi ya Mweka Hazina kwa kila Kanda. Katika kipindi cha mwaka 1985 – 1997 kulikuwepo jumla ya Kanda 16. Mwaka 1998, baada ya Sinza kuwa Parokia, zilibaki Kanda 11. Kuanzia Januari 2007 baada ya Mikocheni kuwa Parokia inayojitegemea, Parokia ya Mwenge sasa inazo jumlaya Kanda nane (8) ambazo zote zina majina ya watakatifu.

12.3 UONGOZI WA JUMUIYA NDOGONDOGO ZA KIKRISTU (JNNK)
Juhudi za kuanzisha JNNK katika Parokia ya Mwenge zilianza kuonekana mapema hata kabla Mwenge haijawa Parokia. Mnamo tarehe 18 Desemba 1977, Jimbo lilitoa mwongozo na semina juu ya umuhimu wa JNNK. Katika semina hiyo wajumbe watatu kutoka Kigango cha Mwenge; Nd. Peter Masaiya (Mwenyekiti); Nd. Paul Njoka (Mweka Hazina) na Ndugu Simon Nnimbo (Katibu) walihudhuria. Baada ya hapo, Kigango kilifanikiwa kuanzisha JNNK kuanzia Kanda moja hadi nyingine. Baadhi ya Wakristu kutoka Kanda hizo ziliendelea kwa Wakristu kukutana na kuelezana mambo mbalimbali ya kiimani na kimaendeleo hadi mwaka 1996 ambapo jumuiya ya kwanza ya Mt. Yosef Mfanyakazi ilipozinduliwa tarehe 15 Agosti 1996 ndani ya eneo lililojulikana kama “Mwenge Shuleni” katika Kanda ya 43 Mwenge Kijijini. Uzinduzi ulifanywa na paroko wa mwenge, Mheshimiwa Padre Krystian Golisz SDS, katka sherehe maalum iliyofanyika nyumbani kwa mmoja wa wanajumuiya hiyo.

Kuanzia mwaka 1997 juhudi Zaidi za kuendeleza na kuzindua JNNK ndani ya Parokia ziliongezeka. Katika taarifa ya utendaji ya mwaka 1997, iliazimiwa kwamba mwaka 1998 uongozi wa maeneo ya Kanda ungeimarishwa zaidi ili ndani ya kila Kanda maeneo yapewe majina ya Watakatifu badala ya majina ya “kienyeji” yaliyokuwa yakitumika. Halmashauri iliona kwamba hatua hiyo ingesaidia jitihada zilizokuwa zinafanywa na uongozi wa Parokia kuanzisha rasmi JNNK. Hata hivyo, kulingana na Katiba ya Halmashauri Walei Katoliki Tanzania (marekebisho ya pili) uundaji rasmi wa JNNK ulifanyika na kukamilika mwezi Novemba 1998, kwa kila jumuiya kufanya uchaguzi wa viongozi wanne, wakiwemo: Mwenyekiti; Makamu Mwenyekiti; Katibu na Mweka Hazina. Katikakikao cha Halmashauri Walei Parokia, kilichofanyika tarehe 18 Oktoba 1998, kilitoa maagizo kwamba uchaguzi wa viongozi hao ufanyike na kukamilika ifikapo tarehe 28 Novemba 1998 ili kutoa nafasi ya kutosha kwa ajili ya uzinduzi wa jumuiya Kikanda. Aidha kikao kilipokea na kukubali ushauri wa Paroko Msaidizi, Padre Jude Massawe SDS, kwamba majina ya Watakatifu somo wa jumuiya hizo yatokane na Watakatifu wa miezi Kikanda. Mpango huo ulilenga kusaidia kuhakikisha kwamba majina ya watakatifu katika jumuiya mbalimbali hayafanani na hivyo kuondoa utata wa ugonganishi majina wakati wa kusoma misa ndani ya jumuiya husika.

 Kutokana na uamuzi huo, Kanda zilipewa uhuru wa kuchagua majina ya Watakatifu somo kuendana na miezi, kati na Januari hadi Novemba kama ifuatavyo: Makumbusho Flats (Januari); Kanda 47 (Februari); Makumbusho Kijijini (Machi); Mikocheni Kanda A (Aprili); Mikocheeni Kanda B (Mei); Mwenge Jeshini (Juni); Kanda 43 (Julai); Kanda 46 (Agosti); Kanda 44 (Septemba); Kanda ya Mlalakuwa (Oktoba); na Mikocheni Kanda STAMICO (Novemba). Uzinduzi rasmi wa jumuiya nyingi ulifanyika mwezi Desemba1998 kwa upande wa kanda za Mikocheni. Mwaka wa 1999 (Januari na Februari), wakati wa uongozi wa Padre Jude Massawe SDS zilizinduliwa JNNK upande wa Kanda za Mwenge. Baada ya kuzinduliwa na kupewa majina ya somo Watakatifu kwa mujibu wa miezi ya kalenda ya mwaka iliyotajwa hapo juu, jumuiya zilianza kustawi kwa kasi kubwa.

Hadi tarehe 10 Novemba 2002 kulikuwepo jumla ya JNNK 114 ambazo zilikuwa hai. Hata hivyo, wakati huo zilikuwa zinafanyika juhudi za kubaini maeneo ambayo yalihitaji marekebisho kwa lengo la kuwa na dadi ya jumuiya zinazowiana na mwongozo wa Jimbo wa kila jumuiya kuwa na familia katiya nane (8) hadi kumi na tano (15) au ishirini (20). Hii ni kumwezesha kila mwanajumuiya kuwa na uhusiano wa karibu zaidi na jirani yake. Wanajumuiya hukutana kwa zamu, kila juma mara moja kwa mwanajumuiya mwenzao ili kusali na kufanya ibada ya Biblia pamoja, kulingana na mwongozo wa Parokia uliotolewa na Jimbo kwa kupitia mtaalamu wa JNNK. Mtaalamu huyo, Sr. Maximilla, alifika Mwenge mwaka 1999 na 2000 kutoa mafunzo kwa viongozi wote wa JNNK kuhusu jinsi ya kuanzisha, kuimarisha na kuendesha ibada za jumuiya. Kabla ya kuanzishwa kwa JNNK uongozi wa Halmashauri Walei ulijikita katika sehemu kuu nne: Ngazi ya Parokia, Kigango, Kanda na Eneo/mtaa). Wakati huo, maeneo kadhaa ndiyo yaliyounda Kanda. Vivyo hivyo, Kanda kadhaa ziliunda Kigango au Parokia. Madhalan huko nyuma ilielezwa kwamba Kanda A – E, kwa maana ya Sinza Vitalu A - E ndivyo viliunda Kigango cha Sinza ambacho hatimaye kikawa Parokia ya Mt. Bikira Maria Mama wa Mwokozi, Sinza.

Katika taarifa ya mwaka 2003, Parokia ya Mwenge iliripotiwa kuwa na jumla ya JNNK 116 zilizokuwa hai. Mwaka 2006, baada ya Mikocheni kuwa Parokia, Parokia ya Mwenge ilibakiwa na JNNK 94. Hali kadhalika, hadi sasa (2018)  Parokia ya Mwenhe ina Kanda nane (8) na kila Kanda ina wastani wa JNNK kati ya 10 na 16 isipokuwa Kanda moja ina Jumuiya tatu (3) na Kanda mbili zina Jumuiya mbili (2) kila moja. Jumla ya Jumuiya zilizoko ni 79, huku idadi ya familia/kaya kwenye kila Jumuiya ikiwa ni kati ya 8 - 15, ijapokuwa nyingine zimekuwepo za familia kati ya 16 - 22.



KANDAMAJINA YA SOMO WATAKATIFU wa KANDAIDADI YA JUMUIYA
1
Kanda 43Mt. Monica12
2
Kanda 44Mt. Yosefu Mfanyakazi14
3
Kanda 46Mt. Yohane Paulo16
4
Kanda 47Mt. Yosefina Bakitha16
5
Kanda ya MlalakuwaMt. Antony wa Padua14
6
Kanda ya Mwenge JeshiniWat. Petro na Paulo Mitume3
7
Kanda ya Makumbusho KijijiniWat. Perpetua na Felisita2
8
Kanda ya Makumbusho FlatsMt. Ritha wa Kashia2

    

JUMLA YA KANDA NI 8 NA JUMUIYA NI 79 79

12.4 IDADI YA WAAMINI
Jumla ya Wakristu katika Parokia hutokana na taarifa zilizopokelewa Parokiani kutoka kwenye Kanda na JNNK ndani ya Kanda hizo. Takwimu hizo zitakuwa sahihi kwa kipindi hicho zinapopokelewa, lakini ieleweke kuwa daima kuna wahamiaji au wahamaji toka nje na ndani ya Parokia kwenda sehemu nyingine na wengine aghalabu hufariki dunia na wengine kuzaliwa.
Mwaka 1985 idadi ya waam

JE UNATAFUTA

PAROKIA?

Upate majibu yako haraka zaidi
Ramani ya Parokia
Hakuna ramani kwa sasa...
Kuhusu Kanisa Katoliki

Ofisi ya Halmashauri ya Walei Jimbo Kuu la Dar es salaam inapatikana makao makuu ya Jimbo,
Kanisa la St. Joseph, barabara ya Sokoine na Manseld street.

P.O Box 167, Dar es Salaam, Tanzania
Tel: +255 762 024 199
Email: mawasiliano@waleijimbodaresalaam.org
            darwaleijimbo@yahoo.com
Web: www.waleijimbodaresalaam.org

Kwa Habari kemkem za Kanisa jiunge nasi

Andika email yako hapo juu, na upokee taarifa za H/walei

Copyright © 2025. All Rights reserved by H/Walei Jimbo Kuu la Dar es salaam