PAROKIA YA UPANGA


SALAMU ZA PAROKO

Mwaka huu (1996), Parokia ya Upanga inatimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Hili ni tukio kubwa sana katika historia ya Parokia yetu.

Wanaparokia wote wana haki na wajibu wa kumshukuru Mungu kwa yote aliyowajalia, hadi kufikia kipindi hiki. Huu ni wakati muafaka wa kutathmini uhai wa Parokia yetu, hasa kuhusu uhusiano na upendo kati yetu na Mwenyezi Mungu, na pia kati yetu sisi wenyewe, ili utusaidie kuweka mikakati thabiti itakayotuwezesha kuingia mwaka 2000 kama Familia ya Mungu inayowajibika kikamilifu, na inayosimama katika misingi ya haki, amani, upendo na ukweli.

Ingefaa tuendelee kutambua udhaifu wetu, na hivyo kujisalimisha kabisa mikononi mwa Mungu, ili kwa njia ya Roho Mtakatifu, aongoze maisha yetu Bikira Maria Mkingwa Dhambi ya asili, aliye msaada kamili wa Wakristu.

Katika kuadhimisha Jubilei hii, tujitahidi kukarabati dhamira zetu, ili zituwezeshe kuamua kwa usahihi yale yanayompendeza Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Sisi ni Kanisa, kusanyiko la kiibada, Mwili wa Kristu, ambamo Yeye ndiye Kichwa. Hii ndiyo sababu kubwa iliyotuwezesha kuziweka nafasi ya mbele kabisa shughuli za Katekesi na za Ibada mbalimbali katika maadhimisho ya Jubilei yetu.

Kwa vile Kanisa pia ni Jumuiya ya watu wanaoishi Ulimwenguni, inatulazimu tutumie wakati huu kuandaa mipango na mikakati madhubuti, ya kuinua hali ya Parokia yetu na kupanua huduma za Kanisa, hasa kwa wenye shida.

Nawatakieni sherehe zenye furaha, wakati sote tukijiandaa kuingia muhula mpya wa miaka 25 mingine ya uhai wa Parokia yetu.

Pd. Mario Maccarini,
PAROKO
.


KUANZISHWA KWA KANISA LA MARIA IMAKULATA, UPANGA

UTANGULIZI

Parokia ya Upanga ilizinduliwa rasmi na Muadhama Kadinali Laurean Rugambwa, mwaka 1971. Kabla ya hapo, ilikuwa Kanisa dogo (Chaplaincy), la Jumuiya ya Waitaliano waliyokuwa wakiishi Jijini Dar es Salaam. Baadaye, Kanisa hili lilijumlisha Wakristu wengine wa eneo la Upanga, hasa wenye asili ya Kigoa, Wazungu na Waafrika wachache waliyoishi katika maeneo hayo wakati huo.

Umuhimu wa kuanzishwa kwa Parokia ya Upanga ulitokana na kuongezeka kwa Waumini Wakatoliki katika maeneo ya Upanga, na kutokana na kutokuwepo Kanisa la karibu maeneo hayo. Muadhama Laurean Kadinali Rugambwa, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, alizungumza na Uongozi wa Jimbo, pamoja na Shirika la Makapuchini, na kukubaliana kulipa Kanisa la Upanga hadhi ya Kiparokia, mwaka 1971, wakati huo kukiwa na Waumini zaidi ya 2,000. Kwa sasa, Parokia ya Upanga ina Waumini zaidi ya 4,500.

Kabla ya kujengwa Kanisa la Upanga, Wakristu waishiyo eneo hili walikuwa wakisali katika Kanisa Kuu la Mt. Yosefu.

Ujenzi wa Kanisa la Maria Imakulata ulitokana hasa na kuwepo kwa Waitaliano wengi, waliyokuwa wakifanya kazi mbalimbali Jijini Dar es Salaam. Idadi kamili haijulikani, lakini inakisiwa walikuwa zaidi ya 500.

Kipindi hicho, kulikuwa na Padri Angelo Simonetti wa Shirika la Makapuchini, ambaye aliletwa nchini mwaka 1957, kuhudumia Waitaliano Wakatoliki, nchini kote, kituo chake kikiwa Parokia ya Mt. Yosefu. Mwaka 1966, Padri Angelo aliomba sehemu ya kujengwa Kanisa katika maeneo ya Upanga. Kwanza alipewa sehemu ambayo kwa sasa kumejengwa Kituo cha Vijana Wakatoliki, Don Bosco Youth Centre, ambacho kinaendeshwa na Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco.

Kutokana na sehemu hiyo kuwa ndogo, Shirika hilo liliongezewa sehemu, ambako Kanisa la Mt. Maria Imakulta limejengwa sasa. Kwa wakati huo, eneo hili lilikuwa ni pori na kiunga cha minazi cha hayati Mzee Tambaza.

Parokia ya Upanga ipo kwenye eneo linalojumlisha Kata za Upanga Mashariki na Upanga Magharibi, katika Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.Kwa upande wa mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, kaskazini inapakana na Parokia za Oyster Bay, Hananasifu na Magomeni. Upande wa magharibi inapakana na Parokia ya Msimbazi, na kusini inapakana na Parokia ya Mt. Yosefu.

Kimipaka, eneo la Parokia ya Upanga linaanzia Selander Bridge, na kufuata Mto Msimbazi hadi Barabara ya Morogoro, kasha linafuata Barabara ya Morogoro kuelekea mjini, hadi Msikiti wa Wahindu. Kuanzia kwenye Msikiti huo kuelekea upande wa kushoto na kufuata bonde dogo la Kisutu hadi baharini, kwa kupitia kwenye Makao Makuu ya Chama cha Msalaba Mwekundu. Pia, kuna vituo vitatu vya ibada katika Parokia: Muhimbili, Betania na Don Bosco, ambavyo huendesha Misa kila siku kwa Wakristu wa maeneo hayo.

Kwa sababu za kihistoria, Parokia hii pia ni kituo (Procura) cha Mapadre na Watawa wa Kapuchini, kinachohudumia Parokia za Jimbo Katoliki la Dodoma.

UHAI WA PAROKIA

Parokia ya Upanga ni kati ya Parokia za zamani katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kwa rehema za Mungu, idadi ya waumini wanaoshiriki katika Ibadan a shughuli mbalimbali za Parokia, imekuwa inaongezeka kila mwaka. Pia, sehemu kubwa ya waumini wanafanya juhudi za kufahamiana na kuungana katika shughuli za Ibada (k.v. kusali Rozari Takatifu, Ibada za Katekesi n.k.), katika mitaa yao.

Wazazi na walezi wanajitahidi kutekeleza miongozo mbalimbali ya Parokia kuhusu taratibu za huduma za Kanisa, hasa zile zinazohusu Sakramenti, k.v. Ubatizo, Komuniyo ya Kwanza, Kipaimara na Ndoa. Wanaparokia wameendelea kutambua nafasi pamoja na wajibu wao katika Parokia. Hii imejidhihirisha katika ongezeko la sadaka wazozitoa siku za Jumapili, na pia katika vipindi mbalimbali vya Kanisa, k.v. wakati wa Kwaresma, Majilio, Noeli na Pasaka.

KAMATI YA LITURGIA NA MAFUNZO YA DINI

Kamati hii, ambayo Mwenyekiti wake ni Paroko, inashughulika na mafundisho ya dini, hasa mashuleni. Mafundisho hayo hutolewa na Padre, Masista, Mabruda na baadhi ya Walei. Pia, kamati hii hujihusisha na Sunday School, Ibada ya watoto wadogo ambao hawajafikia umri wa kupata Kumuniyo ya Kwanza. Ibada hii huendeshwa na akina mama na kina baba wa Parokia yetu, kila Jumapili, kuanzia saa tatu na nusu asubuhi hadi saa tano asubuhi. Kamati hii pia husimamia shughuli za vyama mbalimbali vya kitume vilivyo hapa Parokiani.

Kamati hii husimamia shughuli zote zinazohusu Ibada. Shughuli hizo ni pamoja na kuweka utaratibu unaohusu Ibada mbalimbali zinazoendeshwa Kanisani, k.v. uandaaji wa ratiba za Ibada katika vipindi mbalimbali vya Kanisa, utoaji wa huduma Kanisani na kuratibu shughuli za kwaya.

HALMASHAURI YA PAROKIA

Parokia inalo Baraza la Walei lenye wajumbe 34 wliochaguliwa kutoka maeneo mbalimbali ya Parokia, ambao ni akina mama na akina baba. Sehemu kubwa ya wajumbe hawa wanawakilisha mitaa wanakokaa, na waliobaki wanawakilisha vikundi mbalimbali vya kiroho k.v. WAWATA na VIWAWA. Vikao vya Baraza vinahudhuriwa na Baba Paroko pamoja na Msaidizi wake na Masista wawili, ili kufanikisha mawasiliano na kuimarisha ushirikiano unaotakiwa katika shughuli zote za Kanisa.

BARAZA HUTEKELEZA SHUGHULI ZAKE KWA KUTUMIA KAMATI ZIFUATAZO:

A. KAMATI YA FAMILIA NA VIJANA
Hujihusisha na uimarishaji wa familia na malezi ya vijana. Kamati hii imefanikiwa kufuatilia na kurekebisha ndoa ambazo hazikufungwa kwa taratibu na misingi ya Kanisa. Pia, kamati hii huandaa shughuli mbalimbali zinazokutanisha familia Katoliki hapa Upanga, ili kujenga ufahamiano.

Kamati hii huandaa sherehe ya familia, ambayo hufanyika mara moja kwa mwaka, kabla ya kipindi cha Majilio. Huandaa pia semina, filamu na mihadhara kuhusu masuala muhimu yanayogusa maisha na mienendo ya Wakristu katika nyakati zetu.

Parokia ya Upanga in Jumuiya mbili za Neo-Katekumenato zilizoanzishwa mwaka 1987 na 1992, kwa lengo la kuwamarisha washiriki kiimani, kwa njia ya katekesi. Jumuiya ya kwanza yenye wanajumuiya 35, na Jumuiya ya pili yenye wanajumuiya 70, hukutana kila Jumatano kwa Ibada (Karamu) ya Ekaristi, kuadhimisha Siku ya Bwana.

Wanajumuiya wote hukutana kwa kuishi pamoja mara moja kwa mwezi, kusali na kujenga
moyo wa upendo na uelewano kati yao.

B. KAMATI YA UONGOZI

Kamati hii, ambayo Mwenyekiti wake ni Mwenyekiti wa Baraza, hushirikiana na Paroko kupanga na kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Parokia na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Parokia. Kamati hii ni kiungo kati ya Kamati za Utekelezaji na Baraza katika masuala yote yanayohusu mapato na matumizi ya fedha za Parokia. Na pia masuala yasiyohusiana moja kwa moja na shughuli za kamati nyingine.

C. UMOJA WA WANAWAKE WAKATOLIKI WA TANZANIA (WAWATA)

Parokia ina tawi la WAWATA lenye wajumbe wapatao 35. Shughuli za WAWATA hapa Parokiani ni pamoja na:

(i) Kuendesha Sunday School kwa kushirikiana na Masista.
(ii) Kuandaa na kuendesha sherehe za za Krismasi kwa ajili ya watoto wadogo.
(iii) Kuandaa na kuendesha tafrija za watoto wakati wa Komuniyo ya Kwanza na Kipaimara.
(iv) Kuendesha shughuli mbalimbali, k.v. ‘sale,’ kupata fedha za kuendesha Tawi la WAWATA, na pia kununulia mahitaji kwa ajili ya wagonjwa mahospitalini.
(v) Kushiriki katika utoaji wa huduma Kanisani.
(vi) Kupanga na kuratibu duru za kusali Rozari kwenye nyumba za wanaparokia.

D. UMOJA WA VIJANA WAFANYAKAZI TANZANIA (VIWAWA)

Tawi la VIWAWA limeanzishwa upya mwaka 1989 baada ya kuzorota muda mrefu. Tawi hilo, kwa kushirikiana na Baraza, huandaa programu ya mwaka inayoeleza shughuli za vijana Parokiani katika kuimarisha imani yao na kujenga moyo wa upendo na ushirikiano kati yao.

E. CHAMA CHA MOYO MTAKATIFU WA YESU


Tawi la Chama cha Moyo Mtakatifu wa Yesu lilianzishwa hapa Parokiani mwaka 1987. Hivi sasa, Tawi lina wanachama wapatao 9, ambao licha ya uchache wao wanashiriki kikamilifu katika Ibada zinazisisitizwa katika Jumuiya yao, usafishaji wa mazingira ya Kanisa, kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa.

F. KWAYA

Kwaya ya kwanza ya Parokia, ambayo kwa sasa ina washiriki wapatao 30, iliundwa upya mwaka 1986, kwa kushirikisha watu wazima na vijana. Kwaya ya pili iliundwa upya mwaka 1995, kwa kushirikisha zaidi vijana. Kwaya hii ina washiriki wapatao 15, na licha ya uchanga wake, inaendelea vizuri chini ya usimamizi wa Brother Pius.


MAPAROKO WA UPANGA, TOKA 1970-1996

1970 - Pd. Angelo Simonetti, Paroko wa Waitaliani wa kwanza na wa mwisho.

1970-1974 Pd. Edwardo Saracini

1974-1983 Pd. Alexander Merighi

1983-1994 Pd. Leonard Amadori

1994- Pd. Mario Maccarini

Mapadre wa Kwanza wa Parokia ya Upanga (1970)
Pd. Edwardo Saracini – Paroko
Pd. Angelo Simotti – Msaidizi wa Paroko

Mapadre Walioko Upanga kwa Sasa
Pd. Mario Maccarini – Paroko
Pd. Stanislaus Mancarelli – Paroko Msaidizi

BARAZA LA HALMASHAURI YA PAROKIA


Baraza la kwanza la Halmashauri ya Parokia lilikuwa la kuteuliwa, na liliundwa tarehe 21 Machi 1971. Liliongozwa na Mzee Michael Clement kama Mwenyekiti, na Ndugu A. Braganza kama Makamu wa Mwenyekiti. Ndugu G. Dias alikuwa Katibu; Bibi Franco, Katibu Msaidizi; Brother Edmund, Muweka Hazina, na Ndugu L. Mtalo, Muweka Hazina Msaidizi.

Wajumbe wa Baraza Walikuwa:

Bibi Z. Rigon
Ndugu Kilmurray
Ndugu F. De Souza
Ndugu R. Robo
Ndugu Francis
Ndugu F. Scopece

BARAZA LA KWANZA LA HALMASHAURI YA PAROKIA LA KUCHAGULIWA, LILIUNDWA TAREHE 18 JUNI 1972. LILIKUWA NA WAJUMBE 24.

Waliochaguliwa kuliongoza Baraza hilo walikuw ni:
Mzee Michael Clement – Mwenyekiti
Dr. D. Milinga – Makamu wa Mwenyekiti
Bi N.M. Mclaughlin – Katibu
Ndugu W. Giusseppi – Katibu Msaidizi
Sister Bruna – Muweka Hazina
Ndugu F. Fernandes – Muweka Hazina Msaidizi

WENYEVITI WA BARAZA LA HALMASHAURI YA PAROKIA – MWAKA 1971-1986

Mwaka 1975-1976 – Mzee Michael Clement
Mwaka 1976 – Dr. D. Milinga
Mwaka 1976-1977 – Mzee Anselm Lyander
Mwaka 1977-1987 – Ndugu Eugene Kiliwa
Mwaka 1987-1991 – Ndugu Benedict Kasege
Mwaka 1991-1995 – Ndugu B. Kasege
Mwka 1995-mpaka sasa – Ndugu B. Kasege

WAJUMBE WA SASA WA HALMASHAURI YA PAROKIA

1. Ndugu B. Kasege – Mwenyekiti
2. Ndugu P. Shirima – Makamu Mwenyekiti
3. Ndugu F. Mushumbusi – Katibu
4. Ndugu M.X. Kayombo – Katibu Msaidizi
5. Ndugu Joe Pereira – Muweka Hazina
6. Padre Mario Maccarini – Paroko
7. Padre S. Mancarelli – Paroko Msaidizi

8. Rose Mlipano
9. Thecla Kasege
10. Christine Masiaga
11. Mary Mapindi
12. Francis Fernandes
13. E. Massawe
14. Augusta Fernandes
15. George B. Ndibalema
16. E. Rutahindurwa
17. Felix T. Maliti
18. Marsneta F. maliti
19. Andrea Masiaga
20. F.F. Rutahindurwa
21. D.C. Mwemezi
22. Stephen Rweikiza
23. Zestha Lyimo
24. Eugene B. Kiliwa
25. Patrick Shomari
26. Bernard Kimalando
27. Jane Maginga
28. Sr. Brigitta
29. Stefano Malisa
30. Cossie Msaki
31. Magdalena Gama
32. J. Ojiki
33. A. Mwanjisi
34. Victoria Ezekiel
35. J. Fernandes

MASISTA WALIOISHI PAROKIA YA UPANGA

Masista wa kwanza walikuwa wa Ivere (SCIC), Shirika la Moyo Safi wa Maria, tangu mwaka 1969-1973:
Sr. Asunta – Sista Mkubwa
Sr. Maria Canzi
Sr. Bruna
Sr. Adella
Sr. Raphaela

Mwaka 1973-1978
Sr. Carla
Sr. Rosalia

Mwaka 1978, Walikuja Masista wa Mt. Gemma Galgan (ESG):
Sr. Gaetana – Sista Mkubwa
Sr. Gamarosa
Sr. Irmina
Sr. Ancila
Sr. Valentina

Masista Wakubwa Waliofuata:
1978-1980 – Sr. Ancilla
1983-1985 – Sr. Benedicta
1985-1992 – Cricifisa
1992-1995 – Sr. Damira
1995 – Sr. Angela Brigitta

Masista Walioko Parokiani kwa Sasa:
Sr. Angela Brigitta – Sista Mkubwa
Sr. Maria Rosa
Sr. Maria Veneranda
Sr. Maria Teresilia
Sr. Rose Silvana

Mwenyezi Mungu ameishawaita Masista wawili wa Mt. Galgan waliowahi kutumikia Parokia ya Upanga. Nao ni Sr. Maria Lucy (1987), na Sr. Maria Valentina (1994).

Bruda Pius Nkilagomva amehamishiwa Parokia ya Upanga mwaka 1995, kutoka Parokia ya Kibakwe, Dodoma, ili asaidie katika mafundisho ya dini, Parokiani na mashuleni, na pia kusimamia shughuli za vijana. Kwa kipindi kifupi ambacho amekaa Parokiani, amekuwa karibu sana na vijana. Amewahamasisha na wamejitokeza katika shughuli mbalimbali Parokiani, na kuanzisha kwaya ya vijana, ambayo inaimba katika Misa ya kwanza.

IDADI YA WAKRISTU WA PAROKIA YA UPANGA, 1971-1996

Parokia ya Upanga ilipozinduliwa ilikuwa na Wakristu wapatao 2,500. Idadi ya Wakristu imekuwa ikiongezeka na kufikia 4,500 kwa sasa. Wakristu waliobatizwa katika Parokia ya Upanga mwaka 1971, ni 105. Wakristu wote waliobatizwa Parokia ya Upanga toka mwaka 1971 hadi 1996, ni 1,782. Wakristu waliopewa Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Upanga tangu 1971 hadi 1996, ni 1,219. Wakristu waliofunga ndoa katika Parokia toka 1971 hadi 1996, ni 225.


SHUGHULI ZA IBADA
(Na Eugene Kiliwa)

IBADA za pamoja Kanisani ni moja ya viungo vikubwa vya Wanaparokia wa Upanga. Kilele cha Ibada hizi ni Misa za Jumapili (mbili kwa lugha ya Kiswahili na moja kwa lugha ya Kiingereza).

Katika miaka ya karibuni, kumekuwa na ongezeko la kuridhisha kuhusiana na mahudhurio katika Misa za Jumapili na viwango vya sadaka zinazotolewa katika Misa hizo, na hivyo kuridhisha uhai wa Parokia yetu, licha ya vikwazo vingi vinavyotokana na msongamano wa shughuli za maisha ya kila siku, na pia hali ya maisha ambayo inaendelea kuwa ngumu mwaka hadi mwaka.

Mahudhurio katika ibada za siku za kawaida za wiki bado ni ya chini, ingawa kuanzia mwaka huu (1996), idadi ya waumini wanaohudhuria Misa za kila siku asubuhi, imeongezeka maradufu.

Ndugu wa Jumuiya ya Neo-Katekumenato hukutana kila Jumatano na Jumamosi kwa ibada ya neno la adhimisho la Ekaristi. Hali kadhalika, wanachama wa vikundi vya Biblia hukutana kila Jumamosi jioni kutafakari neno la Mungu.

Parokia ya Upanga ni kati ya Parokia zilizofufua maandamano ya kiibada kuzungukia mitaa mbali mbali ya Parokia. Maandamano hayo hufanyika mara tatu kwa mwaka katika sikukuu ya Matawi, Mwili wa Damu Takatifu ya Yesu na Sikukuu ya Somo wa Parokia (Bikira Maria Mkingwa wa Dhambi ya Asili), yakiwashirikisha waumini wote.

Hata hivyo, bado ipo haja ya kurekebisha mpangilio wa Ibada hizi, ili kwa siku zijazo ziweze kuwashirikisha kikamilifu zaidi waumini wanaotumia lugha ya Kiingereza ambao huwa vigumu kuyangojea maandamano hayo yanayofanyika baada ya Misa Kubwa ya tatu.

Pia, bado kuna haja ya kuhimiza na kuimarisha ushirikishwaji wa waumini wote katika sala na nyimbo, wakati wa Ibada zote za pamoja, ili wasibaki kama wasikilizaji na watazamaji tu wa yale yanayotokea.

Kuhusu huduma zitolewazo Kanisani, utaratibu unaofuatwa ni ule wa zamu ya kila mwezi kati ya akina baba, akina mama na vijana. Kila kikundi huandaa wasomaji, wakusanyaji na wapelekaji wa sadaka. Pia, kila inapowezekana, wanafamilia hupeana zamu ya kupeleka mapaji wakati wa Misa za Jumapili.


SHULE YA CHEKECHEA
(Na Donatian Mwemezi)

Shule hii ilisajiliwa kama kituo cha kuangalia watoto wadogo mchana (Daycare Centre), tarehe 14 Aprili 1973. Wakati huo, Bwana Afya wa Jiji aliruhusu kuandikishwa watoto wasiozidi sitini (60), kufuatana na huduma zilizokuwepo. Kadiri huduma zilivyoongezeka, na idadi ya watoto iliongezeka mpaka kufikia mia na hamsini (150) mwaka 1983. Kutokana na shule za namna hii kuwa nyingi katika Jiji, kwa sasa idadi ya watoto haizidi 80 kwa wakati mmoja.

Watoto wanaopelekwa shuleni hapo ni wenye umri wa miaka mitatu (3) hadi sita (6). Shule ilipoanza, ada ilikuwa Shilingi ishirini (20/-) kwa mwezi kwa kila motto, na kama mzazi alikuwa ana zaidi ya motto mmoja, wa pili alilipiwa Shilingi kumi na tano (15/-), na wa tatu na kuendelea alilipiwa Shilingi kumi (10/-) kwa mwezi. Ada hii imekuwa ikiongezeka kufuatana na hali ya uchumi.

Uongozi wa shule upo chini ya Halmashauri ya Parokia, lakini uendeshaji wa siku hadi siku upo chini ya walimu watatu (sista mmoja na walei wanawake wawili), wakisimamiwa na Paroko.

Hawa watotot wadogo wanafundishwa kuhesabu, kuchora maumbo mbali mbali, kuandika herufi moja moja na kuziunganisha, kuimba, kusali, na maeneo machache ya lugha ya Kiingereza.

Wakati wa kufundishwa darasani, huwa watoto wanatengwa katika makundi mawili au matatu, kufuatana na uwezo wa kuelewa pamoja na umri.

Licha ya masomo ya darasasni, watoto hupata fursa ya kucheza pamoja kwenye viwanja vilivyopo nje na hupewa maziwa, uji mwepesi wa mchele uliochanganywa na mchicha/karoti. Huko nyuma, vyakula kama vile unga wa maziwa, mchele na mafuta ya kupika, vilipatikana bure kutoka kwa wafadhili (mashirika ya misaada), hasa ya Ulaya, lakini kwa sasa misaada hii haipatikani.

Kutokana na sababu hii, vyakula vya watoto hawa vinanunuliwa kwenye soko huria kwa bei za juu. Kwa sababu hiyo, ada inabidi zipande karibu kila mwaka, kukidhi mahitaji haya.

CHRISTIAN PROFESSIONALS OF TANZANIA (CPT)
(Na Theonestina Rweikiza)

1) NI NINI)
CPT ni chama cha kitume cha wanataaluma Wakristo, Tanzania, kilichoanzishwa mwaka 1983, na kusajiliwa chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Chama hiki hujumuisha Wakristo wote ambao wameandaliwa kwa mafunzo maalum, ili kutumia ujuzi walio nao kutoa huduma kwa manufaa ya wote. Kama chama cha kitume, CPT hufanya kazi chini ya mwamvuli wa Baraza la Walei Katoliki Tanzania, ili kutekeleza utume wa walei kwa mujibu wa hati za Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikani.

2) MADHUMUNI
Kwa njia ya utume huu, wana CPT, kama kikundi, au mmoja mmoja, hupataa wasaa wa:-

i) Kujitafiti upya Ukristo wao kwa mwanga na neno la Mungu.
ii) Kushiriki katika jamii ili kuishi maisha ya Injili, kwa kusaidia kuwaimarisha watu wengine
kiroho na kimwili.
iii) Kuyaelewa kitaaluma matatizo mbali mbali yaliyomo katika jamii, nchini kwetu na
ulimwengu mzima, ili kutoa mchango wa kuyatatua, kwa lengo la kuwaondolea watu dhiki na dhuluma, na kujenga jamii yenye haki, upendo na amani

3) CPT UPANGA
Chama cha Parokia ya Upanga (CPT Basic Group), ni kichanga. Parokia ya Upanga ilianzisha rasmi kikundi hiki mwaka 1995, chini ya uwenyekiti wa Bibi Zesta Lyimo. Ingawa kiparokia chama hiki hakijapata msisimko mkubwa, wapo wana CPT wakongwe Parokiani ambao wanshikilia nyadhifa na majukumu ya CPT kitaifa, kama Bibi Elizabeth Massawe (Mtunza Fedha, CPT Kitafia), Bibi Mary Mwingira (Katibu Mkuu wa CPT Kitaifa) na Pd. Vic Maesian anayekaa Mtaa wa Mindu, ambaye ni Mshauri wa CPT Kitaifa.

Aidha, Parokia ya Upanga inatambua na kujivunia CPT ngazi ya Taifa, kwa juhudi zake za kuhamasisha na kushirikisha waumini wa Parokia ya Upanga, katika tafakari na mijadala mbali mbali ya kina, inayohusu jamii, kwa manufaa ya jamii. Tokea mwaka 1988, Parokia yetu imeshirikiana kwa karibu zaidi na CPT kuandaa semina, warsha au mafunzo, ili kushirikishana katika mada na tafakari zifuatazo:-
-Sera ya Serikali ya Idadi ya Watu (Population Policy)
-Vipi tujenge jamii upya
-Matatizo ya rushwa, upotevu na wizi wa mali ya umma
-Matatizo ya uchumi na ustawi wa jamii, miongoni mwa wakulima, akina mama, vijana na familia
-Pia, CPT ilifikia uamuzi wa kutafuta mbinu za kumsiadia na kumwezesha mwananchi kuelewa haki na mamlaka yake kisiasa, kwa njia ya kujitegemea, kupitia program ya elimu ya demokrasia shirikishi, waumini wa Upanga walihamasishwa kutumia haki yao ya kuwachagua viongozi wanaofaa, wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 1995.

MWISHO
Pamoja na pongezi za dhati kwa Parokia ya Upanga kutimiza miaka 25, CPT inawaomba wanaparokia wazidi kupata neema za Mwenyezi Mungu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Pia, CPT inatoa mwaliko kwako wewe mwanataaluma wa Upanga kutafakari kwa makini na kwa unyenyekevu, katika huduma yako kumtukuza Mungu, kutoa uamuzi wa kujiunga na ndugu kumtukuza Mungu, kutoa uamuzi wa kujiunga na ndugu wanataaluma , Wakristo wenzako, ili uweze kutoa mchango wako kujenga Kanisa ambalo ni chumvi, mwanga au taa ya jamii ya Kitanzania na ulimwengu mzima kwa ujumla, ukitumia taaluma yako uliyojaliwa na Mungu.



KWAYA YA PAROKIA YA UPANGA
(Na Donatian Mwemezi)

KWAYA ya Kanisa la Upanga ilianzishwa na Sista Geitana, mara baada ya kuzinduliwa Parokia mwaka 1971, akiwa na vijana ishirini ambao wazazi wao walikuwa washiriki wa karibu katika shughuli za Parokia. Sista huyu ndiye alikuwa mwalimu wa kwaya, na kila Jumapili kabla ya Misa ya kwanza na ya tatu, alifundisha nyimbo chache za Ibada kwa waumini wote.

Kwaya hii ya vijana ilikuwa inaimba katika Misa zote mbili, yaani ya kwanza nay a tatu. Wengi waanzilishi wa kwaya hii wamehamia sehemu nyingine za nchi au jijini, baada ya kumaliza shule na kuanza maisha ya kujitegemea, wakiwa wameoa au kuolewa. Baadhi ya waanzilishi wa kwaya ya Upanga ni Gaudence Nombo, Marehemu Patrick George, Prisca Ojiki, Fransisca Mwaluli, Victoria Max, Barnabas Kiliwa, Bernard Galinoma, Kasambala na Esther Clemence. Mpiga kinanda alikuwa ni Seven Mganza.

Uongozi wa Parokia ulivunja kwaya ya vijana mwaka 1984, kutokana na matatizo ya nidhamu. Kwa muda ambao kwaya mpya ya mchanganyiko wa vijana na wazee ilikuwa bado inaandaliwa, Kamati ya Liturujia ilisimamia shughuli za nyimbo kwa wote katika kila Misa za Jumapili. Ni wakati huu ambapo nyimbo za Kilatini ziliimbwa sana.

Septemba mwaka 1995, kwaya yenye muundo mpya wa mchanganyiko wa wazee na vijana ilianzishwa, na ndio inaendelea mpaka sasa. Mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa Mzee S.J. Nombo, na baadaye Ndugu Donatian Mwemezi alichaguliwa Mwenyekiti mpaka sasa, kikiwa ni kipindi chake cha tatu. Uchaguzi wa uongozi hufanyika baada ya miaka mitatu. Tatizo sugu la kwaya limekuwa ni uchache wa wanakwaya na mahudhurio hafifu. Kwa sasa, kwaya hiyo ya mchanganyiko huwa inaimba katika Misa ya tatu tu. Kwa kutambua kwamba Misa ya kwanza nayo ina waumini wengi kama Misa ya tatu, imeanzishwa kwaya ya vijana wapatao 20 mwaka huu 1996, kwa ajili ya Misa hii, chini ya uongozi wa Bruda Pius wa Shirika la Kikapuchini.


USHIRIKA WA MOYO MTAKATIFU WA YESU
(Na Rose Mlipano)
Ushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ulianzishwa Parokiani Upanga mwanzoni mwa mwaka 1989, chini ya uwenyekiti wa Ndugu Stephen Magessa, ukiwa na wanachama 13. Tarehe 1 Julai 1988, wanachama walipokelewa rasmi kwenye Ibada ya Misa. Mwaka uliofuata, Ndugu Magessa alihama Parokiani na Mama Rose Mlipano alichaguliwa kuchukuwa nafasi yake.

Ushirika huo ulivunjwa mwaka 1990, kutoakana na wanachama wengi kushiriki katika Ibada za Padre Mkwera, ambazo hazikubaliki na Kanisa.

Ushirika wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ulianzishwa upya tarehe 25 Februari 1996, na wanachama 12 na uongozi mpya uliochaguliwa ni: Mama Rose Mlipano (Mwenyekiti), Ndugu T. Ngotta (Katibu), Maria Pius (Katibu Msaidizi), Mama Kimiti (Mweka Hazina) na Mama M. Goyi (Mweka Hazina Msaidizi).

Shughuli za ushirika ni pamoja na kuabudu Ekaristi, Misa Takatifu na kusali kwa pamoja kwa siku zilizopangwa, kutembelea wagonjwa hospitalini na majumbani, kuwasaidia wagonjwa kwa hali na mali na kusoma vitabu vitakatifu, hasa Biblia.


PAROKIA YA UPANGA NA VIJANA WAKE
(Na Victoria Ezekiel)

KATI ya mwaka 1972, Parokia ya Upanga ilipata kundi la vijana waliounda kikundi cha kwaya, wengi wao wakiwa watoto wa wanaparokia wakati huo.

Kundi hili liligawanyika katika sehemu mbili – vijana wafanyakazi na vijana wanafunzi. Kati ya mwaka 1974 na 1983, wakati Parokia ikiwa na Paroko wa pili, Padre Alexander Merighi, kundi la vijana lilizidi kukuwa na kuimarika katika mambo mbali mbali, kwa kuwa Paroko huyu alikuwa na karama na vipaji vya usanii kama vile uchoraji, upambaji na uigizaji.

Kwa hiyo, mambo haya yaliwavuta vijana wengi ambao walizidi kujiunga. Katika miaka ya 1979-1980, liliundwa kundi la vijana chini ya uongozi wa Fr. Merighi, ili kufanya igizo la mchezo wa Mateso ya Yesu Nazareti, na mchezo huu ulivuma sana kwa jinsi ulivyokuwa ukiigizwa kiufundi, na hasa kwa kuwa pia na vifaa vilivyoendana na igizo hilo, kama vile mavazi na michoro iliyochorwa, kuashiria tukio.

Vile vile, ustadi uliokuwa ukifanywa na vijana hawa waigizaji, hasa kijana George Mulamula, ambaye alikuwa akifurahisha sana kwa uigizaji wake kama Yesu wa Nazareti. Katika kipindi hiki pia, uongozi wa vijana ulizidi kukuwa, hasa pale alipoletwa Msaidizi wa Paroko, Padre Santino (ambaye sasa ni marehemu), ambaye naye kwa karama zake alikuwa kivutio kikubwa sana kwa vijana. Parokia ilisaidiwa na Mapadri hawa kupatiwa wafadhili kutoka nje walioleta vifaa mbali mbali vya michezo kuwezesha vijana kukaa muda mwingi parokiani, na hili likawaepusha vijana wengi kushawishika na mambo mengi ya kidunia. Lakini kadiri miaka ilivyopita, ndivyo mambo yalizidi kubadilika.

Vijana wengi ilibidi walazimike kuhama Parokia, ama kwa ajili ya masomo nje ya Parokia, kupata uhamisho kikazi ama kuolewa na wengine kuoa. Hivyo, kundi likaanza kupungua, lakini halikufa kwa sababu vijana walioendelea kubaki walikomaa sana katika nyayo za Mapadri Merighi na Santino. Kwa mfano, vijana Patrick George, Charles Mtabwa, Deus Masota, George Ndibalema, Steven Kiliwa na Deogratias Mhumbira, na wengine wengi waliongoza vijana wenzao.

Kama ilivyo mipango ya Mungu, penye furaha na mafanikio hapakosi matatizo na majonzi. Mwaka 1990, Parokia ya Upanga ilipata pigo kubwa ilipompoteza Patrick George, aliyeugua kwa muda mfupi na kufariki dunia. Vijana walitetereka kidogo, lakini Mwenyezi Mungu akawasimamia na kuwaimarisha vijana wakongwe waliobaki, na kuendelea kuwahamasisha vijana wenzao. Katika miaka ya 1989-1991, Parokia ililazimika kuunda tawi la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA). Chama hiki kiliingia Tanzania mwaka 1959 kwa nia ya kuhamasisha vijana wafanyakazi katika kutoa huduma za Kanisa, na pia kujiendeleza wenyewe katika kazi zao.

Kutokana na mazingira ya Parokia hii, shughuli mbali mbai za vijana na VIWAWA Parokiani, hazijafikia kiwango cha kuridhisha nah ii inatokana na kukosekana kwa ajira na nafasi za kujiendeleza kielimu na kiujuzi, hivyo kusababisha vijana wengi kujiengua katika shughuli za Kanisa.

Hata hivyo, kwa nguvu za Mwenyezi Mungu, wapo vijana waanzilishi na wapya ambao wameendelea na moyo wa kujitolea na kuhamasisha wenzao katika huduma za Kanisa na kuimarisha uhai wa Vijana Parokiani.

Wakishirikiana na Uongozi wa Parokia, Paroko, Baraza la Walei na Walezi wao, Vijana hao wamekuwa wakijumuika pamoja katika shughuli za Kanisa na wamehudhuria semina mbali mbali na kutafakari pamoja Neno la Mungu, uimbaji wakati wa Misa, michezo ya maigizo wakati wa sherehe mbali mbali Parokiani, na kushiriki katika michezo mbali mbali Parokiani na nje ya Parokia.

Ukweli huu umedhihirishwa wazi mwezi Oktoba mwaku huu, pale ambapo Vijana wa Upanga walipojinyakulia ushindi wa kwanza katika mchezo wa mpira wa meza kwenye Tamasha la Don Bosco (Don Bosco Youth Festival) na kwa mantiki hii, tuna tegemeo kubwa la vijana wengi kuhamasika na kujiunga na wenzao. Kwa hivi sasa, mipango iko mbioni kuunda timu ya netiboli na yimu ya mpira wa miguu ya Parokia.


KUTOKA WAWATA
(Na Elizabeth Massawe)

Katika miaka 25 ya kipindi cha Jubilei pamoja na Jubilei yenyewe, wakina mama wamekuwa wakiendelea kuyatakatifuza malimwengu kwa kushirikiana na waumini wengine Parokiani na Jimboni. Baadhi ya viongozi wa zamani wa WAWATA Parokiani ni Mama Milinga, Mama Cathalina Lutayangirwa, Mama Gabriella Kato, Mama Damian Kato na Mama Elizabeth Twissa. Katika kipindi cha miaka sita iliyopita, ushirikiano wa kamati ya utendaji umekuwa kama ifuatavyo:

Jane Maginga, Makamu Mwenyekiti, ambaye kwa sababu ya kuwa masomoni alisaidiwa na Magreth Rulegura. Muweka Hazina ni Agnes Mwanjisi na Makatibu ni Christina Masiaga, akisaidiwa na Theonistina Rweikiza. Baada ya uchaguzi wa 1994, Katibu akawa Victoria Ezekiel, akisaidiwa na Christina Masiaga. Mjumbe wetu Jimboni ni Elizabeth Mbwillo.

• Uongozi ni utumishi katika shamba la Bwana. Kipindi hiki tulifanikiwa kukutana na kujadili mambo mbali mbali, kama vile:
• kutunza familia bora
• uzazi wa mpango kwa njia za asili
• wajibu wa mwanamke Mkatoliki
• sera za ongezeko la watu
• elimu ya demokrasia shirikishi kabla ya uchaguzi mkuu
• uhamasishaji wa kupiga kura
• sinodi ya Afrika
• haki na amani katika familia

Katika malezi, kina mama waliendelea na kufundisha shule ya Jumapili kwa watoto wadogo ambao hawajaanza bado mafundisho ya Komunio ya Kwanza. Kina mama wameshirikiana na Masista na Mapadre katika kutoa elimu ya malango, au unyago kwa Wanakatoliki vijana wa Kipaimara. Kila mwaka wakati wa Noeli huwaongoza watoto kutoa sadaka na zawadi kwa Mtoto Yesu, na hatimaye kuwasindikiza kuzipeleka kwa watoto wenzao mahospitalini au kwenye vituo mbali mbali kama Msimbazi.

Katiba yetu inatuongoza kushirikiana na vyama vyote vya kitume chini ya Baraza la Walei. Hivi muda wote wanawake wamefanya hivyo na kipindi cha uongozi katika baraza, asilimia 49 ya wajumbe ni wanawake. Hivyo kamati zote kiutendaji zina asilimia kubwa tu ya wanawake.

Parokia ina shule ya watoto wadogo kwa ajili ya kuwalea kimaadili na kuwaandaa kielimu kabla ya kuingia shule ya msingi.. Hapo napo asilimia 85 ya walezi ni wakina mama. Mikakati huwekwa kulingana na mahitaji na kulishauri Baraza.

Vipindi mbali mbali, kina mama kwa kujivunia umama, wameandaa na kufanikisha sherehe za ushemasi/upadrisho kwa vijana wetu kadhaa waliopita hapa kwa mwaka wao wa kiuchungaji. Hawa sasa ni Mapadre hodari wa Jimbo wenye uhusiano wa karibu na Parokia.

Jambo la kujivunia katika kundi la wanawake wa Parokia, tunaye Mwenyekiti aliyepita, Mama Elizabeth Twissa, ambaye ni Muweka Hazina wa WAWATA Taifa. Vile vile, ni Mjumbe wa umoja huo ulimwenguni. Hayo ndio matunda ya miaka 25 ya Parokia yetu.

Kupongezana na kufarijiana katika furaha na huzuni
WAWATA tulipotokewa na wenzetu Sista Maria Valentina katika ajali ya gari, akirejea kutoka mafunzo huko Dodoma, na Sista Maria Lucy, aliyeugua muda mrefu na kufariki nyumbani huko Dodoma. Hawa wote tulishirikiana nao kwa muda mrefu katika malezi ya watoto wadogo, Komunio na Kipaimara. Jitihada zao na kujitoa kwao kwa dhati kulitupa moyo sana. Wenzetu wengine waliotutoka hatuwezi kuwataja majina, lakini ni wajibu wa wakina mama kushirikiana na kuzikana.Raha ya milele uwape, Ee Bwana…

Sista Concifissa, aliyekuwa Mama Mkubwa wakati tunaanza uongozi, alitimiza miaka 25, 1993 na tulimpongeza. Yeye alihamishwa kwenda Dodoma na baada yake alikuja Sista demira Joseph, ambaye naye alirudi Dodoma, tukapewa Sista Anjela. Wote hawa tunawashukuru kwa mchango wao mkubwa kwa umoja wetu.

Masista majirani wa Canosa, Benediktini, Salvatori n.k., wamekuwa washiriki wakubwa katika kuboresha huduma Parokiani. Sala za pamoja na ushauri wao umetusaidia sana. Sanamu moja tunayotumia kwa sala za rozari majumbani, tulizawadiwa na Masista wa Canosa. Tunawaombea moyo wao huo na juhudi zao za kuwapa elimu vijana wetu mashuleni, uendelee.

MWISHO
Miaka ishirini na mitano ni kipimo cha kutosha kuona ukomavu kiimani, utashi, maandeleo na mazingira. Tathmini yetu katika kipindi hiki cha uongozi inatupa moyo kiasi katika ukomavu. Pamoja na kwamba mahudhurio ya ushirikiano ni makubwa kati ya wanawake.

Changamoto za maisha, ushindani wa kiuchumi na mapigano ya kiroho yanaongezeka, na hasa kwa jamii yetu iliyoko mjini. Vijana wetu wana tunu tofauti za maisha, kioo cha Kanisa kinachafuliwa na teknolojia ya kisasa.



ANGALISHO

Ni tunu (thamani) zipi sisi wakina mama tunawapa watoto wetu? Je, ni umimi, utajiri, majidekezo ya mwili, starehe bila kazi? Tutavuka mwaka 2000 hivi, na itakuwaje? Katika mwanamke alikuja Mkombozi kwake yeye na dunia ilipata matumaini. Bikira Maria alishiriki, ndio maana aliona mahitaji ya watu. Kwa UPENDO WA KRISTU, TUMTUMIKIE MUNGU KWA USHIRIKIANO.


MPANGO WA KUWAENDELEZE VIJANA WA PAROKIA YA UPANGA

Mnamo mwezi Machi 1995, wakati wa matembezi ya Kiuchungaji Parokiani Upanga, Mhashamu Polycarp Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alipata nafasi ya kuzungumza na vijana wa Parokia ya Upanga kuhusu matatizo yao. Mazungumzo yalikuwa mazito na yalichukuwa muda usiopungua saa moja.

Katika mambo waliomueleza Mhashamu Askofu Mkuu, kwa uchungu, ni malalamiko kwamba Taifa limewatupa, limewasahau, hasa katika swala la ajira. Vijana walimueleza Mhashamu Askofu Mkuu kwamba tumaini lao kubwa limebaki kwa Kanisa tu. Kama Kanisa nalo likiwatema, basi hawajui nani atawatetea au kuwaokoa.

Maneno ya vijana hao yalimchoma sana Mhashamu Askofu Mkuu na aliiagiza Halmashauri imtayarishia mpango kamilifu wa kuwasaidia vijana kutokana na matatizo mazito yanayowakabili vijana, hasa ya ajira.

Halmashauri ya Parokia imelichunguza kwa ndani tatizo la vijana kuanzia ngazi ya Taifa, na kutokana na sense iliyofanyika hivi karibuni, imeonekana kuwa Parokia ya Upanga ina vijana 175 wasiokuwa na ajira, na kati a hawa wavulana ni 66 na wasichana ni 109. Wengi wao wamemaliza shule ya msingi (darasa la saba), lakini wapo vijana walimaliza hata vyuo vikuu wasiokuwa na ajira.

Juhudi zinafanyika kuwatafutia kazi vijana 12 ambao wana elimu ya juu au ujuzi maalum (skills), mahali popote itakapowezekana, na kuwaendeleza kielimu na kiujuzi wenye elimu ya chini, kwa kutumia vyuo mbali mbali vilivyopo katika Parokia za Jimbo, pamoja na vyuo vinavyomilikiwa na Serikali au madhehebu mengine na mashirika mbali mbali (NGOs).

Pia, kuna mpango wa kuanzisha mfuko wa maendeleo ya vijana wa Parokia ya Upanga katika azma ya kutekeleza mpango huo, ambao kutumika kwake kutategemea zaidi ushirikiano na msaada wa hali na mali kutoka yeyote mwenye nia njema.


SHUKRANI
Kamati ya Historia ya Jubilei inatoa shukrani za dhati kwa wote walioshiriki na kufanikisha maandalizi ya sherehe za Jubilei ya Parokia yetu ya Upanga.

Shukrani ziwafikie:
Halmashauri ya Parokia na wanaparokia kwa mchango wao wa sala, hali na mali, katika kufanikisha maandalizi ya sherehe za Jubilei ya Miaka 25 ya Parokia.

Shukrani za pekee tunazitoa kwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Polycarp Pengo kwa uongozi wake wa kitume na ushauri wa pekee kwa uongozi wa Parokia ya Upanga.

Aidha, shukrani za pekee tunazitoa kwa Baba Paroko, Mario Macarrini, kwa usimamizi thabiti wa Parokia, na msaada wa kiroho kwa wanaparokia pamoja na ushirkiano mzuri na viongozi wa Parokia, Mapadri, Masista, Bruda na Halmashauri ya Parokia, katika shughuli mbali mbali.

Tunaomba pia tutoe shukrani za pekee kwa Padri Barnaba Maddii (OFMCP), wa Shirika la Wafransisko Wadogo wa Kapuchini, kwa mchnago mkubwa katika ujenzi wa uzio na ukarabati wa Kanisa, katika kipindi kifupi aichokaa Parokiani.

Shukrani kwa Kamati ya Maandalizi ya Sherehe za Jubilei, chini ya uongozi wa Paroko na Mwenyekiti, Benedict Kasege, kwa kazi yao nzuri, mchango wao na moyo wa kujituma, ambavyo vimekuwa msingi wa kufanikiwa kwa maandalizi ya sherehe za Jubilei. Tunaomba tueleze kutambua kwetu mchango mkubwa wa Maporoko, Mapadri, Masista na Viongozi wote waliotumikia Parokia hii, ama kwa kuianzisha au kwa kuiendeleza na kuiacha katika hali nzuri, hali ambayo inatuwezesha kusherehekea miaka 25 ya Parokia yetu leo.

Mwisho, shukrani zinatolewa kwa waliochangia kufanikisha kuchapishwa kijitabu hiki.

Imekuwa vigumu kuweza kuingiza historia na matukio yote yaliyotokea Parokiani katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, na kwa usahihi. Lakini tunaamini kuwa kumbukumbu hii ni sehemu kubwa ya muhtasari wa historia ya yale tuliyoweza kukusanya, na tunaamini itakuwa kumbukumbu nzuri kwa wanaparokia watakaopenda kujua, angalau kwa muhtasari, historia ya Parokia yao.

Tunawatakia kila la heri katika kusherehekea miaka 25 ya Jubilei ya Parokia.


Srephen Rweikiza,
Mhariri/Mwenyekiti wa Kamati ya Historia,
Jubilei ya Parokia ya Upanga


JE UNATAFUTA

PAROKIA?

Upate majibu yako haraka zaidi
Ramani ya Parokia
Hakuna ramani kwa sasa...
Kuhusu Kanisa Katoliki

Ofisi ya Halmashauri ya Walei Jimbo Kuu la Dar es salaam inapatikana makao makuu ya Jimbo,
Kanisa la St. Joseph, barabara ya Sokoine na Manseld street.

P.O Box 167, Dar es Salaam, Tanzania
Tel: +255 762 024 199
Email: mawasiliano@waleijimbodaresalaam.org
            darwaleijimbo@yahoo.com
Web: www.waleijimbodaresalaam.org

Kwa Habari kemkem za Kanisa jiunge nasi

Andika email yako hapo juu, na upokee taarifa za H/walei

Copyright © 2025. All Rights reserved by H/Walei Jimbo Kuu la Dar es salaam