Historia ya H/walei Jimbo
HISTORIA YA M IAKA 50 YA HALMASHAURI WALEI TANZANIA (1969 – 2019)
UTANGULIZI:
1. Tarehe 24 June, 2019 Halmashauri ya Walei Tanzania itatimiza Miaka 50 tangu ianzishwe.
Chombo hiki cha Walei katika Kanisa kimekuwa na nguvu ya kukoleza utume wa Walei kwa kutumia karama zao, kuanzia Jumuiya ndogondogo za Kikristo, Jumuiya ya Mtaa, Kitongoji, Kanda, Parokia, Jimbo hadi Taifa. Haya yote ni matokeo ya Mtaguso wa II wa Vatikani, katika hati yake kwa Walei inayosema “wanaonyesha utume wao kwa matendo yao, kwa kueneza Injili na kwa kutakatifuza watu na kupenyeza na kukamilisha mambo ya kilimwengu kwa roho ya Injili. Kwa njia hii matendo yao ya kilimwengu yanaweza kutoa ushahidi wa Kristo na kuleta wokovu wetu. Kwa vile maisha ya mlei yamo katika masuala ya kijamii katika ulimwengu, anaitwa na Mungu kujawa roho ya Kristo na kutumia utume wake katika malimwengu akiwa kama chachu ya Ulimwengu”.
Uongozi wa Halmashauri Walei huanzia Jumuiya Ndogondogo za Kikristu (JNNK) hadi Taifa. Uongozi huu huitwa kamati tendaji za halmashauri Walei mahalia (JNNK, Mtaa, Kitongoji, Kanda, Parokia, Jimbo na Taifa).
1.1 Wajibu wa jumla wa viongozi wa Halmashauri Walei katika ngazi zote ni:
* Kwa kushirikiana na Hierakia kudumisha Utume wa Walei na kuimarisha maisha ya kitakatifu miongoni mwa Walei, na kuwahimiza Walei kushiriki katika kuujenga Mwili wa Kristo.
* Kustawisha utume wa familia na Uinjilishaji wa kina.
* Kushauri na kushiriki katika ujenzi wa Kanisa mahalia.
* Kujenga na kudumisha moyo wa sala na ibada sahihi miongoni mwa Walei.
* Kustawisha vikundi mbalimbali vya kitume katika maeneo yao.
* Kushirikiana na uongozi Hierakia katika ngazi yoyote ya Halmashauri Walei katika kutekeleza majukumu ya Kanisa.
* Kuhamasisha shughuli za maendeleo kiuchumi, kijamii na kisiasa kadiri ya mtazamo wa Kanisa.
* Kuwezesha na kushauri juu ya uongozi bora katika jamii.
* Kushirikiana na taasisi na mashirika mengine katika masuala yote ya maendeleo ya binadamu; kiroho, kinafsi, kimwili na kimazingira, kwa kuzingatia taratibu za Kanisa.
* Kushiriki kikamilifu na kwa kutumia miundo iliyowekwa na Kanisa katika kulinda na kutetea uhai, heshima na haki za binadamu.
1.2 Kama chombo cha kueneza utume wa walei, Halmashauri ya Walei Tanzania katika kipindi chake cha Miaka 50 (pamoja na ile Miaka 25 wakati chambo hiki kikiitwa Baraza la Walei Tanzania) kimeendelea kukua na kupanuka, kulingana na msimamo na msukumo wa viongozi wa Kanisa kwa wakati husika.
2. KUANZISHWA KWA HALMASHAURI WALEI TANZANIA.
2.1 Kutokana na msukumo wa mkutano wa Mtaguso wa II wa Vatikani, pamoja na maamuzi na maelekezo ya Mtaguso huu, uongozi wa Kanisa Tanzania, kama mahali pengine ulimwenguni ulianza kutafakari njia mbali mbali kuwashirikisha Walei kikamilifu katika shughuli za Kanisa, ili washike mahali pao kwa kutumia karama zao Mungu alizowapa katika Kanisa inavyositahili.
Juhudi za Kanisa Katoliki Tanzania zilikuwa kupata njia zilizo bora zaidi za kutekeleza utume wa Walei. Makundi yaliyotumika hasa yalikuwa ni vijana, wanawake, wafanyakazi na wasomi.
Mwaka 1967 kulikuwa na mkutano mkubwa huko Roma, mkutano huu ulishirikisha Maaskofu, Mapadre, Watawa na Walei toka pote duniani. Hapa Tanzania waliohudhuria ni Mhashamu Askofu James Sangu, Ndugu Joseph Mtayoba, Ndugu Bernadeta Kunambi na wengine wanne kutoka majimboni. Mkutano
huo ulizungumzia kuhusu kushirikishwa Walei wote katika ujenzi wa Kanisa na mwaka huo huo 1967, Baraza la Maaskofu Tanzania lilibuni mswada wa katiba ya chombo hiki kilichoitwa Baraza la Walei na baadaye kubadilishwa jina kuwa Halmashauri ya Walei. Mswada huo ulisambazwa kwenye majimbo yote kwa ajili ya majadiliano na maoni toka parokiani na majimboni kwa muda wa miaka miwili. Mwaka 1969 Baraza la Maaskofu Tanzania liliitisha mkutano wa wawakilishi wawili wawili kutoka majimboni kote na mkutano huo ulifanyika tarehe 24 June 1969 eneo la Kurasini, na Mhashamu Askofu James Sangu ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa mkutano huo kwa sababu ndiye aliyekuwa Askofu wa utume wa Walei miaka hiyo.
Baada ya majadiliano na maoni iliamuliwa kuwe na chombo cha kukuza na kuendeleza utume wa walei, yaani Baraza la Walei Tanzania ambalo sasa ni Halmashauri ya Walei Tanzania.
Baraza la Walei Tanzania lilibadilishwa kuwa Halmashauri ya Walei Tanzania, kwani ilionekana haiwezekani kuwa na mabaraza mawili; yaani baraza la Walei na baraza la Maaskofu Tanzania. Pia katiba ya baraza la Walei ilifanywa upya na kuwa katiba ya halmashauri ya Walei Mwaka 2000. Baada ya mchakato huo kuisha, katiba hiyo ilitangazwa kuwa Katiba ya Halmashauri Walei Tanzania tarehe 6 Januari 2004.
Halmashauri Walei huendeshwa na walei wenyewe kwa kufuata katiba na ushauri kutoka kwenye Hierakia, na kuwachagua viongozi wao wenyewe.
2.2 Uongozi wa mwanzo kabisa wa Baraza la Walei Tanzania katika uchaguzi wa Mwaka 1969 walipatikana wafuatao:
* Mwenyekiti: Chief Patriki Kunambi
* Katibu Mkuu: Ndugu Joseph Mutayoba
* Katibu Msaidizi: Ndugu Bernadeta Kunambi
* Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu na mshauri wa walei wakati huo: Padre Robert Rweyemamu
Hawa ndiyo viongozi waliotembelea majimbo yote kuhamasisha chombo hiki cha walei.
Halmashauri ya Walei Taifa inatoa shukrani nyingi kwa wote walio jitahidi kusimika /kuanzisha baraza la Walei (Halmashauri ya Walei Tanzania) na viongozi wa kwanza wa chombo hiki.
Kumbukumbu ya majina yao ni kama ifuatavyo:
* Baraza la Maaskofu (TEC) kwa ujumla wake.
* Askofu Mkuu Marko Mihayo.
* Askofu Mkuu Polycarp Pengo.
Wengine ni:
* Askofu Raymond Mwanyika.
* Askofu Renatus Butibubage.
* Chief Patriki Kunambi.
* Bibi Bernadeta Kunambi.
* Ndugu Joseph Mtayoba.
* Ndugu Peter Mahundi.
* Ndugu M. Mwingira.
* Nugu C.E.N. Hagam.
* Padre Robert Rweyemamu aliyekuwa katibu mkuu TEC wakati huo.
2.3 Uongozi wa sasa hivi wa Halmashauri Walei Tanzania ni kama ifuatavyo:
* Mwenyekiti: Ndugu Gasper M. Makiluli.
* Makamu Mwenyekiti: Ndugu Ester Njau.
* Katibu: Ndugu Switbert Malola.
* Katibu Msaidizi: Ndugu Donesta Byarugaba.
* Mtunza Hazina: Ndugu Alvera Kabwogi.
* Mkuu wa Idara: Padre Ubaldus Kidavuri.
* Askofu Mwenyekiti: Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma.
3. MAFANIKIO KUTOKANA NA CHOMBO CHA HALMASHAURI WALEI.
3.1 Tumeshuhudia idadi ya vituo vya sala Vigangoni, Parokiani na Majimboni kuongezeka; ongezeko la walei kutumia uwezo na karama zao katika kulijenga Kanisa; idadi ya vyama vya kitume imeongezeka.
3.2 Kuweza kusajiliwa vyama vya kitume ngazi ya Taifa ambavyo ni;
* Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu.
* UWAKA (Umoja wa Wanaume wa Katoliki).
* Shirika la Wazee na Wastaafu wa Wakatoliki wa Mtakatifu Agustino.
* TYCS (Tanzania Young Christian Students).
* Legio Mariae
* TMCS (Umoja wa Wanachuo Wakatoliki Tanzania).
* CPT (Christian Professionals of Tanzania).
* VIWAWA (Vijana Wakatoliki Wafanyakazi).
* WAWATA (Wanawake Wakatoliki Tanzania).
* Kolping Society of Tanzania.
3.3 Kumekuwepo na mfumo mzuri kupitia Katiba ya Halmashauri Walei kwa ajili ya kuwawezesha viongozi wa Halmashauri Walei kutekeleza shughuli zao kwa urahisi na kikamilifu. Na pia katiba hii inawezesha ushirikishwaji wa walei kikamilifu kwenye kulijenga Kanisa na kutakatifuza malimwengu.
Kadri ya katiba ya Halmashauri Walei, muundo wa Halmashauri ya Walei huanzia ngazi ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo hadi Taifani. Chini ya kamati tendaji kuna kamati ndogo ndogo kila moja ikilenga eneo lake maalumu kama zinavyojieleza hapa chini:
* Kamati ya mipango uchumi na fedha.
* Kamati ya malezi na familia.
* Kamati ya ibada na liturujia.
* Kamati ya elimu ya dini, mafundisho ya Kanisa na Teknolojia.
* Kamati ya Haki na Amani.
3.4 Pia kuweza kujenga na kuanza kutumika kwa kituo cha malezi ya kiroho cha Mwenyeheri Isidori Bakanja kinachosimamiwa na Halmashauri Walei Taifa.
3.5 Halmashauri kupiga hatua Kimataifa kwa kuanzishwa Halmashauri Walei ya Kanda ya Africa ya Mashariki (Council of Lay in Eastern Africa - COLEA) Nchi hizi za ukanda wa Mashariki ni Zambia, Malawi, Tanzania, Uganda, Kenya, Sudani Kusini, Ethiopia, Elitrea na Djibuti.
4. CHANGAMOTO.
4.1 Ni namna ya Walei kuenenda katika swala zima la kutakatifuza malimwengu;
Pamoja na kwamba kumekuwepo na matokeo ya ongezeko kubwa la Walei kushiriki katika shughuli za Kanisa, bila shaka hii ikiwa ni kutokana na msukumo wa Mtaguso wa II wa Vatikani, kuna changamoto katika utendaji wa Walei:
Baada ya kupita Miaka 22 ya Mtaguso wa II wa Vatikani, kulifanyika Sinodi ya Walei Mwaka 1987 kwa nia ya kutathmini utendaji wa Walei katika kanisa. Matokeo ya tathmini hii yanatuambia kuwa, pamoja na Mtaguso wa II wa Vatikani kuleta msukumo kwa Walei kuchukua nafasi zao katika shughuli na maisha ya Kanisa, kumekuwako na vishawishi viwili kwa Walei ambavyo wamekuwa wanashindwa kuvikwepa kama ifuatavyo:
a. Kishawishi cha kwanza ni kile cha Walei kupenda na kujikita mno katika shughuli za Kanisa na kuacha wajibu wao pia wa kuhusiana na malimwengu kadri inavyowapasa.
b. Kishawishi cha pili kwa Walei kimekuwa kutoihusisha Imani na Neno la Mungu katika maisha yao. (Kuisoma tu Injili badala ya Kuiishi).
Sinodi hii ya Walei ya Mwaka 1987 imeeleza na kutoa tahadhari juu ya hatari inayojitokeza kwamba, Walei wanaojitoa kwa maisha ya Kanisa mara nyingi wanajigubika ndani ya Kanisa lenyewe na kuacha majukumu yao ya kijamii, kitaaluma, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Sinodi inaelekeza kwamba, hatuwezi kuugeuza ulimwengu na kuufungamanisha na Mungu kama wanaoamini katika ukombozi wa Kanisa, ama wanaacha uhusiano wao na ulimwengu au wanajuhushisha na na malimwengu bila utakatifu.
4.2 Namna ya Walei kushiriki katika Uinjilishaji.
Kuna changamoto ya namna ya Walei kujipanga katika utekelezaji wa uinjilishaji katika ulimwengu wa leo. Katika changamoto hii, Walei tunatakiwa tuelewe sawasawa kitu kinachoitwa Uinjilishaji Jamii.
Baba Mtakatifu Francis katika Wosia wake wa Kitume; Furaha ya Injili (Evangelii Gaudiu) ametoa tafakari kuhusu mwelekeo wa kijamii wa uinjilishaji ambapo ameongelea maeneo ya msingi yafuatayo: Matokeo ya kijumuiya na ya kijamii ya kerigma; kuwahusisha maskini katika jamii; Manufaa ya wote na Amani katika jamii; Mazungumzo ya kijamii kama mchango kwa Amani.
4.3 Uelewa mdogo na matumizi hafifu ya Katiba ya Halmashauri Walei Tanzania.
Asilimia kubwa ya viongozi wa Halmashauri Walei hasa katika ngazi ya Jumuiya, Kigango na Parokia hufanya shughuli zao bila kuwa na elimu ya kutosha juu ya Katiba ya Halmashauri Walei.
Katika utendaji wao, viongozi wengi hufanya shughuli zao wakitegemea kuongozwa na Mapadre.
Katika Katiba ya Halmashauri Walei kuna kamati ndogo ndogo ambazo haziundwi, na kama zikiundwa hazifanyi kazi kwa sababu kuna uelewa mdogo kwa Walei walio wengi juu ya kamati hizi.
4.4 Ukosefu wa elimu na mafunzo endelevu kwa Walei.
Kumekuwepo na changamoto ya ukosefu wa utaratibu kabambe wa elimu na mafunzo endelevu kwa Walei juu ya imani, wito na utume wao, na namna ya kuutekeleza.
Mpangilio wa semina na mafunzo kwa Walei hautilii maanani vipengele muhimu vinavyohitajika katika kuwaandaa Walei katika kukabiliana na changamoto za utume wao na Kanisa la leo katika ulimwengu wa sasa.
Mtakatifu John Paulo II alitoa mwongozo makini juu ya namna ya kuwaandaa walei katika wasilisho lake la kitume “The Vocation and Mission of The Lay Faithful – A Simplified Text” kutoka sura ya tano (soma na. 57 mpaka 64).
4.5 Kubaki nyuma katika teknolojia.
Kutokana na kuwa nyuma katika maendeleo yanayo husiana na TEHAMA uongozi wa Halmashauri Walei hushindwa kubadilishana taarifa za kiutendaji kwa wakati. Pia hushindwa kusoma kwa wakati miongozo mbalimbali ya Kanisa n.k. kwa wakati muafaka.
4.6 Katika Jumuiya Ndogondogo za Kanisa kuna mahudhurio hafifu ya wakina Baba na vijana.
4.7 Kuna mmonyonyoko mkubwa wa maadili katika jamii.
4.8 Kuyumba kwa Imani kutokana na Utandawazi.
4.9 Sakramenti ya ndoa kuonekana imepitwa na wakati na hii imepelekea vijana wengi kuishi uchumba
sugu bila kubariki ndoa zao na wengi wa walio katika ndoa hawaziheshimu.
5. MIPANGO YA BAADAYE.
5.1 Kuweka mikakati kabambe ya kuwaandaa Walei kutambua wajibu na wito wao katika Kanisa la leo.
5.2 Kutilia maanani juu ya Mtaguso wa II wa Vatikani, na kuuchukulia kama dira ya uhakika wakati Walei wanatimiza wajibu wao katika karne hii ya 21.
Kuzitilia maanani Hati mbili zifuatazo kutoka Mtaguso wa II wa Vatikani;
a. Hati juu ya Fumbo la Kanisa inayojulikana kama Mwanga wa Mataifa (Lumen Gentium).
b. Hati juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa sasa.
Hati hizi mbili ambazo hutazamwa kama ndiyo Mtaguso wenyewe wa II wa Vatikani zina mahusiano yaliyo muhimu sana kwetu katika kulijenga Kanisa la leo. Ni kwamba hati juu ya Fumbo la Kanisa inatufunulia kuwa Yesu Kristo ndiye Mwanga wa Mataifa. Wakati hati juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa sasa inachukuliwa kama mpangilio makini (blue print) kwa ajili ya kuyatekeleza yaliyomo ndani ya hati juu ya Fumbo la Kanisa.
Pia Hati juu ya Walei kutoka Mtaguso wa II wa Vatikani kupewe umuhimu wa juu. Hati hii ni kwa ajili ya kuwaongoza Walei katika kutekeleza utume wao wa msingi wa kutakatifuza malimwengu.
5.3 Uimarishaji wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo (JNNK) na Walei kwa ujumla wao.
Kuweka msisitizo wa kuwepo na kamati zifuatazo kwenye kila ngazi husika, na kutimiza wajibu wao sawa na malengo kusudiwa Kikatiba, na vilevile kujiongeza /kujiboresha kulingana na changamoto zinazojitokeza kwenye wakati / mahali husika:
* Kamati ya mipango uchumi na fedha.
* Kamati ya malezi na familia.
* Kamati ya ibada na liturujia.
* Kamati ya elimu ya dini, mafundisho ya Kanisa na Teknolojia.
* Kamati ya Haki na Amani.
5.4 Kuzitumia fursa zitokanazo na matumizi ya teknolojia kwa ajili ya mawasiliano /vikao, kubadilishana taarifa, mafundisho, majarida, mada muhimu, semina, matangazo, malipo /makusanyo ya michango n.k.
5.5 Kutengeneza Website (data base) ya Walei kwa ajili ya kuweka taarifa zetu ili tuweze kutambuana; na taarifa zinazohusu mambo, shughuli, kazi (taaluma) na biashara mbali mbali zinazo tuhusu (kujua talanta zilizoko ndani ya kanisa).
5.6 Kuweka taarifa /shughuli /kazi zote za Kanisa, kwenye database kulingana na ngazi husika; ili iwe rahisi pia kwa Hierakia kuona na kujua kwa urahisi mafanikio au mapungufu yaliyopo kwenye wakati husika; mfano; kuona na kujua mara moja, idadi ya waumini; wangapi wamezaliwa; wamebatizwa; wenye vikwazo; walegevu; wategemezi; walemavu; makusanyo ya michango nk.
5.7 Kuitumia Website (data base) ya Walei kwa ajili ya kutangaziana biashara /bidhaa; ujuzi au taaluma; kupeana maarifa; kushirikishana nk, kulingana na mahitaji ya Walei wenyewe kwa wenyewe. (Ni fursa kubwa sana tuliyonayo wakatoliki kutokana na Uwingi wetu; ama ni soko la pili au la tatu kwa ukubwa duniani baada ya Wachina)
5.8 Kuzitumia fursa zilizopo ndani ya Kanisa zitokanazo na mashirika, taasisi, vyama vya kitume, rasilimali watu, ardhi, majengo, shule, hospitali, maabara, miundombinu mizuri nk, kwa manufaa yetu na Ulimwengu
Walei tunatakiwa kujipanga vema tukishirikiana sisi kwa sisi, Makleri na wenye maisha ya Wakfu, katika kuzitumia vema fursa na karama zilizomo ndani ya Kanisa.
6 HITIMISHO.
Viongozi wa walei na walei kwa ujumla wadumu katika sala na mazoezi mbalimbali ya kiroho na kujiendeleza kielimu ili waweze kuimarika katika utume wao kwa sababu wao ni Kanisa. Watakapotenda
yale yote yanayohusu utume wao wasisubiri kusifiwa bali waseme sisi tu watumwa tusio na faida tumefanya tu yaliyotupasa kufanya. Lk. 17:10
- Matukio
- Juinge na Kanisa
- Neno kuu la mwaka 2018
- Kalenda ya matukio 2018
- Ramani ya Tovuti
- Biblia Mtandaoni na zaidi
- Liturujia ya Kanisa Katoliki
- Mkate wa siku ya LeoLorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore Ut enim ad minim magna aliqua”2 kor 2:16