WANAWAKE WAKATOLIKI TANZANIA - WAWATA
HISTORIA FUPI YA WAWATA 1972-2018
UTANGULIZI
Wakati Kanisa katoliki linapoadhimisha miaka 150 ya Ukristo Tanzania,WAWATA (Wanawake Wakatoliki Tanzania wanatimiza miaka 46 tangu baraza la maaskofu katoliki Tanzania lilipoidhinisha rasmi kuanzisha kwa Chombo hiki ambacho kinawaunganisha wanawawake wakatoliki Tanzania ili kwa pamoja waweze kutoa mchango wao kwa kanisa na jumuiya. Kwa Moyo wa Shukrani WAWATA wanaungana na kanisa zima la Tanzania kumshukuru Mungu kwa ujio wa wamisionari walioleta Enjili ili kutuletea wokovu. WAWATA ni chombo cha kuwaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Muundo wa WAWATA umeanzia katika Jumuiya Ndogondogo za kiKristu, Vigango, Dekania, Parokia, Jimbo hadi Taifa kama ulivyo muundo wa Kanisa Katoliki Tanzania na kila mwanamke Mkatoliki ni mwanachama wa WAWATA. Kimataifa WAWATA ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Duniani (WUCWO-World Union of Catholic Women Organization) iliyoanzishwa mwaka 1910 yenye makao yake makuu huko Ufaransa.
Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kustawisha kanisa na jamii. ( Katiba ya WAWATA, uk. 1 na 2). Ikiwa ni mojawapo ya jumuiya za kanisa, WAWATA inajishughulisha na shughuli zote za kuwaendeleza wanawake kiroho na kimwili waweze kutoa mchango wao kikamilifu katika kujiendeleza kulistawisha kanisa na jamii kwa ujumla katika nyanja za kiroho, matendo ya huruma, uchumi na maendeleo huku ikiongozwa na dhamira yake kuu ya: Kwa Upendo wa Kristo Tutumikie na Kuwajibika (Katiba ya WAWATA, uk. 3-5).
HISTORIA YA KUASISI/KUANZISHWA KWA JUMUIYA YA WAWATA
Vuguvugu la kuanzisha Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania, lilianza rasmi pale
Kipalapala katika Jimbo la Tabora.
Kutokana na mwaliko wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano wa II fursa ilitolewa kwa Walei kutokana na ubatizo wao wajue wajibu wao na wajiweke katika utumishi wa Kristo na wa Kanisa ( Hati ya mtaguso No. 914)
Mwaka 1967 wakati wa mamlaka ya Papa Yohane wa 23 Vatikano Roma iliwashirikisha waumini Wakatoliki duniani wakiwemo maaskofu, mapadre na walei ili kujadili juu ya hali ya kanisa. Tanzania iliwakilishwa na walei kutoka Majimbo manne, wakiwemo:-
Ndugu Joseph Mutayoba kutoka Jimbo la Bukoba, ndugu Selestin Fidelis kutoka Jimbo la Rulenge, ndugu Linus Kisusangi kutoka Jimbo la Iringa na Bibi Bernadete Kunambi kutoka Jimbo Kuu la Dar Es Salaam.
Baada ya mkutano huo Bibi Bernadette Kunambi alishauriwa na Askofu Sangu ahudhurie mkutano wa Wanawake wa Dunia ili kuona na kujifunza, wenzetu wa nchi nyingine wanavyofanya ili tuwashawishi watu wetu nyumbani kuanzisha chama cha akina mama Katoliki. (Nukuu kutoka kauli ya Bibi Kunambi).
Ilipofika mwaka 1968 Wahashamu Maaskofu wa Tanzania waliwaita tena walei kutoka Majimbo yote yaliyokuwepo ili kuzungumza nao jinsi ya kuwashirikisha kikamilifu utume wao.
Kamati iliundwa kuandaa mbinu za utekelezaji wa kuwafikia wakristo wote, chini ya aliyekuwa Mkurugenzi Padre James Sangu (Sasa marehemu) alikuwa Askofu wa Jimbo la Mbeya na uongozi wa Askofu Mkuu Marko Mihayo, Mwenyekiti Askofu Renatus Butibubage. Padre Novatus, ndugu Joseph Mutayoba na Bibi Bernadette Kunambi na Chief Patrick Kunambi alishirikishwa rasmi katika maandalizi ya kuandaa katiba ya walei kama mwongozo wa Utume wao kwa jukumu lililo mbele yao.
Tarehe 20 Juni 1969 ndiyo siku rasmi Baraza la waumini Katoliki lilizaliwa, na tarehe 24 June 1969, Baraza la Maaskofu Katoliki waliipokea katiba ya Walei na kuwaagiza rasmi, katiba hiyo ianze kutumika mara moja. Na jina Barazalikafutwa na kuwa Halmashauri Walei.
Vyama vilivyokuwa hai kwa wakati huo ni Young Christian Students (YCS), Utawa wa Tatu, na chama cha Mt. Vincent wa Paul. Ndoto ya kuanzisha chombo kitakacho washirikisha Wanawake Wakatoliki ilikuwa inawaka moyoni mwa Bibi Bernadette Kunambi.
UHAMASISHAJI WA UTUME MAJIMBONI
Licha ya Bibi Bernadette Kunambi kuteuliwa kuwa Katibu wa Baraza la waumini, lakini ndoto yake ya kuanzisha chombo maalumu kinachoweza kuwaunganisha Wanawake Wakatoliki wenye wajibu wao kama Wanawake katika Kanisa. Ndoto hiyo ilikuwa inaanza kutoa mwelekeo.
Mwaka 1969, kati ya Wanawake wachache waliobahatika kuhudhuria mkutano wa Baraza la Waumini kutoka majimboni, ni Bibi Bernadette Kunambi , Sr. Claudia Mapalala, Bibi Cresentia Jahari, Bibi Anna Haule na Bibi Emiliana Bayo.
Kikundi hicho ndiyo chimbuko la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania. Waliunda uongozi wao Bernadette Kunambi- Mwenyekiti, Sr. Claudia Mapalala- Makamu Mwenyekiti, Anna Haule Katibu, Emiliana Bayo Katibu Msaidizi na Cresentia Jahari Mweka fedha. Waliandaa katiba ya kuwaongoza katika kuhamasisha Wanawake wenzao.
Kazi hiyo haikuwa rahisi hivyo ilitoa changamoto kubwa kwa vile ilikuwa ni jambo geni kimapokeo kama Wanawake. Hofu ilienea kwa Makleri, walei Wanaume na Wanawake wenyewe kutokana na Utume huo mpya ulioingia.
Ilipofika mwaka 1970, vuguvugu la kuhamasisha Wanawake Wakatoliki wautambue wajibu wao katika Kanisa, ulipata sura mpya kabisa. Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki wa ulimwengu (WUCWO) Bibi Pillar Bellasilo na Bibi Carmen Victory, Katibu Mkuu wa WUCWO, walishiriki kwenye semina iliyoandaliwa rasmi na Wanawake Wakatoliki wa Tanzania ili kuwahamasisha akina mama na kuwatia moyo katika Utume huo mpya.
Bibi Mary Hancock na Dr. Schroder, waliungana pamoja na wageni hao kutoka WUCWO, walishirikiana na Bibi Bernadette Kunambi, kuwahamasisha akina mama waone Mtaguso Mkuu kama mkombozi kwao, bila ya kuwaachia wanaume tu kwani kanisa ni la waumini wote na waliwataka wasiogope, kwani hiyo ni kazi ya Mungu. Kwa ushirikiano mkubwa wa Baraza la Maaskofu, kupitia uongozi katika Majimbo yao, na baraza la waumini lililokwisha pata mwanga mkuu, Wanawake Wakatoliki walihamasika na kuupokea wito huo. (Kutoka Muhutasari wa mkutano Mkuu wa Baraza la Waumini 1970).
Juhudi za Bibi Bernadette Kunambi na Wanawake wenzake waliopata nafasi ya kushiriki katika uanzishaji wa Baraza la Walei zilisaidia sana, katika kuweka mambo sawa na mtazamo kubadilika kidogo kuhusiana na masuala mazito ya kanisa na maendeleo yake kiustawi, hivyo kuwafanya Wanawake wawe na sauti. Katika kufanikisha uhai wa kanisa, uhai unaohitaji sayansi na teknolojia, Bibi Bernadette Kunambi alijifunza mengi katika mikutano mbalimbali ya kimataifa na kutembelewa na wajumbe wa WUCWO k.m. Bibi Jacquiline Styut toka Uingereza aliyekuja kuhimiza na kuimarisha uanzishaji wa Wanawake Wakatoliki nchini.
Wahashamu Maaskofu walitoa msaada mkubwa sana kwa uanzishwaji wa Wanawake Wakatoliki kuanzia ngazi ya chini na Bibi Bernadette Kunambi akiwa ndiye Mwenyekiti wa kwanza, alialikwa na Bibi Jacquiline Styut kuhudhuria mkutano wa WUCWO huko Torhout Ubelgiji mwaka 1970. Katika mkutano huo Bibi Bernadette Kunambi alichaguliwa kuwa mjumbe wa kamati tendaji toka Afrika, nafasi liyomfanya autangaze Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania ndani na nje ya Tanzania
Mwaka 1971 Wanawakae Wakatoliki walipata fursa ya kukutana kitaifa ili kuijadili Katiba yao, kuona uwezekano wa kuunda chombo madhubuti kitakacho waunganisha kwa lengo la kutimiza wajibu wao katika kanisa. Mkutano huo ulishirikisha Wanawake wawili wawili kutoka katika kila jimbo na baadaye kuungana na kushiriki semina na mkutano mkuu wa Baraza la Walei.
Baadhi ya masomo yaliyokuwa yanatolewa kwa washiriki wote ni kama ifuatavyo ili kuwaandaa pia kisiasa kwa maendeleo ya nchi.
Wajibu wa waumini katika kanisa - ikisisitizia juu ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikano kuhusu Utume wa Walei NO. 912 no. 1041 Uk 282 311.
Utekelezaji wa majukumu katika kanisa na Jamii.
Sheria ya ndoa ya 1971.
Siasa na uchumi n.k.
Pamoja na kwamba Bibi Bernadette Kunambi alikuwa mwanasiasa aliyebobea, kanisa halikuacha kumtumia katika nafasi yake ya uongozi kama Mkuu wa Wilaya ya Temeke na Ilala na pia katika nafasi yake ya ubunge aliochaguliwa 1971.
Fursa iliyomwezesha kuunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) na Umoja wa Wanawake Tanzania (U.W.T) katika kuhimiza malezi ya watoto/vijana na kuleta maendeleo ya Taifa la Tanzania.
Mbegu iliyopandwa na bibi Bernadette Kunambi ilikuwa changamoto nzuri iliyowaweka Wanawake Wakatoliki sawa na kuwawezesha kuwa na sauti ya utii, usikivu, na unyenyekevu katika kanisa na jamii, walishirikiana na wenzao wa U.W.T. Kwa uhakika ukiangalia huko nyuma tulikotoka, unaona kwamba kazi hiyo ya kuanzisha chombo cha Umoja kinachowashirikisha waumimni wote kuutambua wajibu wao katika kanisa, chombo thabiti na chenye nguvu kiutendaji kiliungwa mkono na Baraza la Maaskofu Katoliki wakatoa baraka zao kuiruhusu WAWATA itumie katiba yao rasmi.
Ilikuwa furaha ya pekee kwa WAWATA mwaka huo 1972 kutambuliwa rasmi na Baraza hilo na kila Mhashamu Askofu katika nafasi yake, katika Jimbo lake, waliweka msingi imara wa kusambaza ujumbe muhimu wa Utume wa WAWATA na maendeleo ndani ya kanisa kwa kutumia katiba hiyo. Kwa kuona umuhimu wa WAWATA katika changamoto na maendeleo ya kanisa, Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa aliridhia kuwapa WAWATA Taifa ofisi ndogo pale St. Joseph kwenye ofisi zake za Jimbo ili WAWATA waendeshe shughuli zao za kitume kwa uhuru.
Utaratibu alioutumia mwadhama ulikuwa chachu kwa wahashamu Maaskofu wengine kuimarisha shughuli za WAWATA majimboni mwao.
Ilipofika mwezi Sept. Tarehe 23 - 26 1972 Wanawake Wakatoliki wapatao 62 kutoka Majimbo yote walikutana tena Kipalapala Tabora, wakafanya semina kujadili juu ya Utume wa WAWATA katika kulinufaisha kanisa pamoja na vyombo vyake, wakamalizia na mkutano Mkuu wa uchaguzi.
Waliochaguliwa rasmi kushika uongozi na kuhamasisha wenzao majimboni ni hawa wafuatao:-
Mwenyekiti - Bibi Bernadette Nampombe Kunambi Jimbo Kuu la Dar Es Salaam
Makamu - Sr. Maria Claudia Jimbo Kuu la Tabora
Mwandishi Anna Haule Jimbo Kuu laTabora
Mweka Fedha Kresentia Jahari Jimbo laSame
Mjumbe - Anna Mtungi - Jimbo la Bukoba
Mjumbe - Honorina Mwakitosi - Jimbo la Dodoma
Mjumbe - Sr. Lidwina Katabi Jimbo la Sumbawanga
Mjumbe Emiliana Bayo Jimbo Kuu la Arusha
(Nukuu kutoka Mkuatano wa WAWATA Kipalapala Tabora June 23 26 Septemba 1972)
Kipindi cha kwanza cha Uhamasishaji kwa Walei/Wanawake Wakatoliki kilikamilika kwa kuitikia mwito wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano II na ujumbe wa kuwa tayari kuimarisha wito huo majimboni. Muundo wa katiba hiyo, umeanzia katika Tawi kwa siku hizi tungesema kwenye jumuiya ndogondogo za Kikristo, Kanda, Kigango, Parokia, Jimbo hadi Taifani na Kimataifa.
Wanawake Wakatoliki walikubaliana kuwa kiingilio chao kiwe ni ubatizo katika kanisa Katoliki, na wamemchagua Mama Bikira Maria msaada wa Wakristo awe somo wao na kusheherekea sikukuu yake mwezi Septemba, kila mwaka ambapo kila mwanamke mkatoliki yuko huru, hana shughuli za kilimo au mavuno shambani
UONGOZI WA WAWATA ULIPO WAKATI WA ADHIMISHO LA MIAKA 150 YA UINJILISHAJI:
Katika kipindi hiki uongozi uliochaguliwa
1. Olive Luena - Mwenyekiti
2. Theodora Mtejeta - Makamu wa Mwenyekiti
3. Desideria Maita - Katibu
4. Sara W.Kessy - Katibu Msaidizi
5. Evaline Malisa - Mtunza Fedha
MAFANIKIO UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WAWATA
Katika mipango yake ya utekelezaji WAWATA imekuwa ikiongozwa na madhumuni ya kuanzishwa kwake. Maswala haya yalipewa kipaumbele Kitaifa na katika ngazi zote za WAWATA kulingana na mazingira yake..Ifuatayo ni orodha ya shughuli na mafanikio ya WAWATA Katika miaka 46 ya uhai wake
(i) Kujitakatifuza ili kutakatifuza-
WAWATA walijihusisha sana na uhuishaji Utume na Uinjilishaji katika ngazi za Jumuiya, Parokia na Majimbo hususani:
Uimarishaji wa Jumuiya ndogo ndogo.
Hija mbalimbali katika maeneo ya hija Tanzania na meneo Matakatifu k.m Nchi Takatifu( Israel) Fatima, Louders, Avila, Rome nk Hija zilizonandaliwa na WAWATA wenyewe kmf. Kibeho Rwanda, Namgongo Uganda, Nyakijoga Bukoba..
Mafungo ya mwaka katika ngazi zote
Vikundi vya sala na ushiriki katika vyama vingine vya kitume
Kukuza miito na kusaidia Seminari kwa hali na mali
Kuanzisha na kulea Utoto Mtakatifu
Matendo ya Huruma kwa wahitaji
Tafakari ya mafundisho ya kanisa katika matukio mbalimbali ya kanisa
(ii). Uinjilishaji katika nyanja za Imani tofauti
WAWATA waliendelea kuwa washiriki wa Mikutano ya Umoja wa Madhehebu mbalimbali kwa ajili ya amani Tanzania (ICRP Interreligious Council of Tanzania)
Kushiriki kila mwaka katika za siku ya Wanawake dunian ( Women World Day of Prayer
(iii). Kumwendeleza Mwanamke Kiuchumi
Kupiga vita Umaskini kupitia Mpango wake wa WASMEP( WAWATA small and Microenterprise) kwa kuwawezesha akina mama wapate mikopo midogomidogo programu ilianza mwaka 1992 na hadi kufikia mwaka 2017 akina mama wapatao 60,000 waliweza kupata mikopo midogomidogo ya kujikimu katika Majimbo Katoliki 32) Programu hiyo imeweza kutoa mafunzo yaliyotolewa kwa viongozi 465 wa WAWATA kutoka majimboni, kuhusu mbinu za kufanya biashara yenye tija, inayozingatia masoko ya uhakika utengenezaji biashara bora zenye kuleta ushindani kuzalisha biashara za kutosha kukidhi soko na wao wenyewe kupata mbinu za kutunza mahesabu/ fedha zao. Mradi huu ulianzishwa kwa kufadhiliwa na HORIZONT 3000 Austria, OPEN HAND- Uswiss na TROCAIRE- Ireland.. Hadi kufikia 2013 Mradi uliendelea vizuri sana na mara baada ya mabadiliko ya uongozi katika ngazi za majimbo kumekuwepo na changamoto nyingi sana katika urejeshaji wa mikopo
(iv). Kuendesha programme/kampeni mbalimbali kufanyika kitaifa na Katika kanda
Kushiriki kikamilifu katika harakati za kumwnua Mwanamke kuptia mikutano ya Umoja wa Mataifa Huko mexoco 1975,Copenhagen 1980,Nairobi 11985 na Beijing 1995 WAWATA walitoa ufadhili kwa kumlipia mama wa Kiislamu kumwezesha kushiriki Mkutano wa Beijing.
Programme endelevu ya kupiga vita gonjwa la Ukimwi
Mafunzo ya Uongozi yaliyofadhiliwa na Justice and Peace ya Baraza la Maaskof Canada na CAFOD ya Uingereza 1985-1995
Tafakari mbalilmbali kuhusu nafasi ya WAWATA katika kanisa na taifa
Mafunzo ya Kitaifa kuhusu Biashara Haramu ya Binandamu ( Human Trafficking ) na sasa semina na mafunzo hayo yanaendeshwa kikanda Tanzania nzima
Utekelezaji wa adhimisho la miaka 40 ya Wawata Pamoja na wa kauli Mbiu ya WUCWO Upendo kwa vitendo love in action
Kushiriki mikutano na makongamano ya AMECEA na Baraza la Maaskofu Tanzania
Haya yote yalitendeka kwa kuzingatia yafuatayo:
Umuhimu wa Amani duniani na hasa katika bara la Afrika
Nafasi ya mwanamke kama mshiriki wa Mungu katika Uumbaji
Kwamba wanawake ni walinzi wa kwanza wa uhai wa binadamu
Kwamba wanawake wengi huishi katika hali ya umaskini
Kwamba WUCWO inasisitiza ujenzi wa amani katika ngazi ya familia, kanisa na jamii
Kwamba wanawake na familia zinaguswa na maumivu na uchungu wa wanafamilia wanaougua na kufa kwa UKIMWI ulioenea kwa kasi barani Afrika
Kwamba wanawake hawashirikishwi ipasavyokatika nafasi za maamuzi katika jamii hivyo ni jukumu la WAWATA Kuwa na Programme za Uongozi n.k
(v) Mafaniko katika kushika nyadhifa Mbalimbali kitaifa na kimataifa
WAWATA wanamshukuru Mungu kwamba licha ya nafasi mbalimbali za Uongozi:
Katika Ngazi ya WUCWO ,Mama Bernadetat Kunambi aliwahi Kuwa Mjumbe wa Bodi na Makamu wa Raisi 1972-1982, Mama Olive Luena ,Mjumbe wa Bodi ya WUCWO 1983-1996 akifuatiawa na mama Elizabeth Twissa Mjumbe wa Boadi na makamu waRaisi bara la Africa 1997- 2014 na sasa Prof.Bertha Koda 2015- hadi 2018
Katika ngazi ya Vatikano , Mama Bernadette Kunambi aliwahi kuteuliwa na Baba Mt. Kwenye Baraza la Kipapa la haki na Amani ( Justice and Peace)kwa miaka Mitano.na mama Olive Luena aliteuliwa na Baba Mt.John Paul11 kwenye Baraza la kipapa la Walei ( Pontifical Council of the Laity) nafasi aliyoitumikia mwaka 1990-1995.
Katika Ngazi ya Kimataifa mwaka 1990 mama Olive Luena alichaguliwa kuwa miongoni mwa maraisi wa World conference on Religion and Peace hadi 1995 chombo kinachounganisha madhehebu yote duniani kwa ajili ya Amani na kufanikiwa kuwa Muasisi wa chombo hicho hapa Tanzania kijulikanacho kama Interreligious Council of Tanzania (ICRPT)
CHANGOMOTO
Zipo changamoto nyingi zikiwemo za kiuchumi na za kijammii ambazo WAWATA kama sehemu ya kanisa na Taifa wanaendelea kupambana nazo katika ngazi mbalimbali . Katika kipindi cha kuandika historia hii changamoto kubwa ni hasa zifuatazo .
Upungufu wa ari ya WAWATA kukubali kujitolea kushika nafasi za uongozi kwa kwa vile hakuna mshahara au posho
Matatizo sugu ya WASMEP ( Mikopo ya WAWATA) ambayo yamesababaishwa na unogozi kutowajibika katika baadhi ya majimbo.
Kutowajibika kwa baadhi ya viongozi katika majimbo hasa katika kuhudhuria vikao na katika kutekeleza maazimio yaliyoafikiwa kitaifa
Mawasiliano finyu na baadhi ya majimbo
- Matukio
- Juinge na Kanisa
- Neno kuu la mwaka 2018
- Kalenda ya matukio 2018
- Ramani ya Tovuti
- Biblia Mtandaoni na zaidi
- Liturujia ya Kanisa Katoliki
- Mkate wa siku ya LeoLorem ipsum dolor sit amet, consectetur adipisicing elit, do eiusmod tempor incididunt ut labore et dolore Ut enim ad minim magna aliquaβ2 kor 2:16