KUHUSU HALMASHAURI YA WALEI
Eneo la Uinjilishaji
Mkuza (Kibaha)
April 2025
MAFUNDISHO

WAJIBU WA KIONGOZI NDANI YA KANISA

Mafundisho na Mwl. Paschal G. Mtaki

Kiongozi ndani ya Kanisa ana jukumu kubwa la kuhakikisha waumini wanaelekezwa katika mafundisho sahihi ya kiimani, kuwa mfano wa maadili mema, na kuhimiza mshikamano wa kiroho. Anapaswa kuwa mnyenyekevu, mwenye hekima, na aliye tayari kuhudumu kwa upendo

YALIYOJIRI

Ili tuwe na utendaji mzuri katika ngazi mbalimbali za Uongozi katika Halmashauri ya Walei na Vyama vya Kitume ni vyema  kila mmoja wetu ajue na atimize "WAJIBU WAKE KATIKA KAZI ZA UTENDAJI NDANI YA KANISA." Viongozi wanawajibu wa kujua kuhusu Utume wa Walei katika ngazi zote, wajue hali ya Kanisa ilivyo sasa, wajue changamoto zinazolikabili Kanisa na utume wao na jinsi ya kuweza kukabiliana nazo. Viongozi wana wajibu wa kuijua IMANI yao, kuisimama na kuitetea. (Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume) Imani yetu imejikita katika misingi mikuu mitatau; Neno la Mungu, Mapokeo matakatifu(Dogma) na Mamlaka funzi

  -  Warumi 10:17 basi Imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa Neno la Mungu
  -  Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga katika njia zangu (Zab 119;105)
  -  Waebrania 11: 1 Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyo onekana

Pasipo Imani haiwezekani kumpendeza Mungu hata katika utendaji wako. Unapopungukiwa Imani omba kwa Mungu (Yakobo 1:5)Katika Kanisa kuna uongozi wa aina mbili;
  a. Uongozi Hiarakia, na  
  b.  Uongozi wa walei

Viongozi Hierakia Ni Wakristo Wakatoliki wabatizwa wenye daraja katika Kanisa Katoliki ambao ni Mashemasi, Mapadre na Maaskofu. Ni Makuhani. Kwa daraja yao Takatifu, Kristo amewakabidhi kazi ya - Kufundisha,  - Kutakasa, - Kutawala katika jina lake na kwa uwezo wake,- Hivyo hawa ndio wenye mamlaka ya kiutendaji katika kanisa  - (Rejea Katekisimu ya Kanisa Katoliki Uk. 222-227)


TATHMINI
MAFANIKIO

Mtaguso Mkuu wa II wa Vatikano ulitilia mkazo ushirikishwaji wa walei katika kazi ya utume wa Kanisa. Unasema walei wana nafasi yao katika maisha ya utume wa Kanisa, utume wao katika jumuiya za kanisa ni wa lazima hivi kwamba bila huo, utume wa wachungaji ni mara nyingi utakosa kuwa na matunda. Kwa kupitia hati juu ya Utume wa Walei (Apostolicum Actuositetam Nr 10), Mababa wa Mtaguso waliona umuhimu wa kuwapa Walei nafasi wanayostahili katika utume wa Kanisa, na kuwataka wajisikie kuwa washiriki wenye uwajibikaji.

(Mtaguso II wa Vatikano, Hati na 12, Dikrii juu ya utume wa Walei,  Na 916 (2) unasema, "Kanisa limeanzishwa kwa lengo la kuwashirikisha  watu wote ukombozi wa wokovu, ambao hupatikana kwa kuenezwa Ufalme wa Kristo duniani pote kwa utukufu wa Mungu".

Mwadhama alizingatia ustawishaji wa utume wa walei Jimboni, hivyo aliimarisha utume huu kijimbo na kiparokia. Kijimbo alimteua Padre kuwa Mkurugenzi wa utume wa walei. Hata mpango wa kuunda Jumuiya Ndogo Ndogo uliweza kufanikiwa pale ambapo walei wameshirikishwa kikamilifu.



CHANGAMOTO
  1. Ni namna ya Walei kuenenda katika swala zima la kutakatifuza malimwengu;
    Pamoja na kwamba kumekuwepo na matokeo ya ongezeko kubwa la Walei kushiriki katika shughuli za Kanisa, bila shaka hii ikiwa ni kutokana na msukumo wa Mtaguso wa II wa Vatikani, Changamoto za kiutendaji wa Walei:, kumekuwako na vishawishi viwili kwa Walei ambavyo wamekuwa wanashindwa kuvikwepa kama ifuatavyo:

    a.  Kishawishi cha kwanza ni kile cha Walei kupenda na kujikita mno katika shughuli za Kanisa na kuacha wajibu wao pia wa kuhusiana na malimwengu kadri inavyowapasa.
    b.  Kishawishi cha pili kwa Walei kimekuwa kutoihusisha Imani na Neno la Mungu katika maisha yao. (Kuisoma tu Injili badala ya Kuiishi).

  2. Namna ya Walei kushiriki katika Uinjilishaji.
    Kuna changamoto ya namna ya Walei kujipanga katika utekelezaji wa uinjilishaji katika ulimwengu wa leo. Katika changamoto hii, Walei tunatakiwa tuelewe sawasawa kitu kinachoitwa Uinjilishaji Jamii.

  3. Uelewa mdogo na matumizi hafifu ya Katiba ya Halmashauri Walei Tanzania.
    Asilimia kubwa ya viongozi wa Halmashauri Walei hasa katika ngazi ya Jumuiya, Kigango na Parokia hufanya shughuli zao bila kuwa na elimu ya kutosha juu ya Katiba ya Halmashauri Walei.

  4. Ukosefu wa elimu na mafunzo endelevu kwa Walei.
    Kumekuwepo na changamoto ya ukosefu wa utaratibu kabambe wa elimu na mafunzo endelevu kwa Walei juu ya imani, wito na utume wao, na namna ya kuutekeleza.

    Mtakatifu John Paulo II alitoa mwongozo makini juu ya namna ya kuwaandaa walei katika wasilisho lake la kitume The Vocation and Mission of The Lay Faithful  Akutoka sura ya tano (soma na. 57 mpaka 64).

  5. Kubaki nyuma katika teknolojia.
    Kutokana na kuwa nyuma katika maendeleo yanayo husiana na TEHAMA uongozi wa Halmashauri Walei hushindwa kubadilishana taarifa za kiutendaji kwa wakati. Pia hushindwa kusoma kwa wakati miongozo mbalimbali ya Kanisa n.k. kwa wakati muafaka.

  6. Katika Jumuiya Ndogondogo za Kanisa kuna mahudhurio hafifu ya wakina Baba na vijana.

  7. Kuna mmonyonyoko mkubwa wa maadili katika jamii.

  8. Kuyumba kwa Imani kutokana na Utandawazi.

  9. Sakramenti ya ndoa kuonekana imepitwa na wakati na hii imepelekea vijana wengi kuishi uchumba sugu bila kubariki ndoa zao na wengi wa walio katika ndoa hawaziheshimu.


NINI KIFANYIKI
  1. Kuweka mikakati kabambe ya kuwaandaa Walei kutambua wajibu na wito wao katika Kanisa la leo.

  2. Kutilia maanani juu ya Mtaguso wa II wa Vatikani, na kuuchukulia kama dira ya uhakika wakati Walei wanatimiza wajibu wao katika karne hii ya 21.
    Kuzitilia maanani Hati mbili zifuatazo kutoka Mtaguso wa II wa Vatikani;
       a.  Hati juu ya Fumbo la Kanisa inayojulikana kama Mwanga wa Mataifa (Lumen Gentium).
       b.  Hati juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa sasa.

    Hati hizi mbili ambazo hutazamwa kama ndiyo Mtaguso wenyewe wa II wa Vatikani zina mahusiano yaliyo muhimu sana kwetu katika kulijenga Kanisa la leo. Ni kwamba hati juu ya Fumbo la Kanisa inatufunulia kuwa Yesu Kristo ndiye Mwanga wa Mataifa. Wakati hati juu ya Kanisa katika Ulimwengu wa sasa inachukuliwa kama mpangilio makini (blue print) kwa ajili ya kuyatekeleza yaliyomo ndani ya hati juu ya Fumbo la Kanisa.

    Pia Hati juu ya Walei kutoka Mtaguso wa II wa Vatikani kupewe umuhimu wa juu. Hati hii ni kwa ajili ya kuwaongoza Walei katika kutekeleza utume wao wa msingi wa kutakatifuza malimwengu.

  3. Uimarishaji wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo (JNNK) na Walei kwa ujumla wao.
    Kuweka msisitizo wa kuwepo na kamati zifuatazo kwenye kila ngazi husika, na kutimiza wajibu wao sawa na malengo kusudiwa Kikatiba, na vilevile kujiongeza /kujiboresha kulingana na changamoto zinazojitokeza kwenye wakati / mahali husika:
        - Kamati ya mipango uchumi na fedha.
        - Kamati ya malezi na familia.
        - Kamati ya ibada na liturujia.
        - Kamati ya elimu ya dini, mafundisho ya Kanisa na Teknolojia.
        - Kamati ya Haki na Amani.

  4. Kuzitumia fursa zitokanazo na matumizi ya teknolojia kwa ajili ya mawasiliano /vikao, kubadilishana taarifa, mafundisho, majarida, mada muhimu, semina, matangazo, malipo /makusanyo ya michango n.k.




Hifadhi ya Mafundisho

Hakuna kumbukumbu ya somo iliyopatikana...