KUHUSU HALMASHAURI YA WALEI
Uongozi
Utawala & Utendaji

   "Jubilei ya miaka 75 ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam - Tufanywe upya na Roho Mtakatifu 

Mhashamu . Stephano Lameck Musomba OSA
Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam
Jimbo Kuu la Dar es Salaam

07 July 2021 - July 2025

Alizaliwa tarehe 25/9/1969 katika kijiji cha Malonji Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, baba yake ni Lameck Musomba mama yake ni Maria Kandonga.

Safari yake kielimu inaanzia katika Shule ya msingi Malonji kuanzia kwaka 1979 hadi mwaka 1985 alipohitimu darasa la saba. Alijiunga na Seminari ndogo ya Maua iliyopo katika Wilaya ya Moshi Vijijini kwa kidato cha kwanza hadi cha sita kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1995. Baada ya hapo alijiunga na Taasisi ya Wasalvatoriani huko Kola Morogoro kwa masomo ya falsafa na teolojia kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2003 na kutunukiwa shahada za awali za falsafa na teolojia

Katika safari ya wito alianza kuvutiwa na wito wa kitawa tangu mwaka 1988 na akaenda kupata uzoefu wa maisha ya kitawa katika Shirika la Waagustiniani (OSA) huko Mahanje Songea. Baada ya hapo alijiunga na upostolanti kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 1998 huko Mahanje na baaadaye huko Morogoro. Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 1999 alipokea majiundo ya unovisi huko Manila Ufilipino. Mnamo tarehe 25/9/2002 aliweka Nadhiri za daima katika Shirika la kitawa la Waagustiniani (OSA) na mwaka huohuo tarehe 9/12/2002 alipata ushemasi katika Taasisi ya Wasalvatoria ambayo kwa sasa ni Chuo kikuu cha Jordan Morogoro. Alipewa daraja takatifu ya upadri tarehe 24.7.2003 huko Mahanje Songea mkoani Ruvuma.

Baada ya Daraja Takatifu ya upadre aliteuliwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mavurunza kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2004. Baada ya hapo alitumwa kwenda kusomea Elimu ya Mababa (Patrology) kuanzia mwaka 2004  hadi mwaka 2008 katika Chuo cha Instutum Patristicum Augustinianum, kilichopo Roma Italia ambako alitunukiwa Shahada ya umahiri (Licentiate) katika Teolojia akibobea katika Elimu ya Mababa (Patrology).

 

Baada ya masomo huko Roma kuanzia mwaka mwaka 2008 mwaka 2009 alikuwa mlezi katika nyumba ya Waagustiniani na Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordani Morogoro. Mwaka 2009 alienda Manila Ufilipino kutoa semina mbalimbali kwa wanovisi, waprofesi na wapostolanti. Kuanzia 2009 hadi mwaka 2015 alikuwa paroko wa kwanza katika Parokia ya Temboni Jimbo kuu la Dar es salaam na wakati huo akiwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro. Mwaka 2015 aliteuliwa tena kuwa Wakili Paroko wa Parokia ya Mavurunza, na Msimamizi wa Jumuiya ya Mtakatifu Monika Mavurunza. Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Paroko wa muda wa Parokia Mtakatifu Ambrose Tagaste Dar es Salaam hadi mwaka 2016.

Kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2019 aliteuliwa kuwa mlezi na Gombera wa Nyumba ya Malezi ya Mtakatifu Agostino iliyopo Morogoro. Kuanzia mwaka huo 2019 mpaka sasa amekuwa ni paroko na msimamizi wa Jumuiya ya Mt. Monika Mavurunza, Temboni na Mt. Rita wa Kashia. Kuanzia mwaka 2008 hadi sasa amehudumu kama Katibu wa Delegation ya Waagustiniani Tanzania.

Askofu Mteule Stephano Musomba ni mzoefu wa kuongea lugha mbalimblai ikiwemo, Kiswahili, Kiingereza, Kiitaliano, kusoma Kispaniola, Kifaransa, Kigiriki, na Kilatini.

Tarehe 7Julai 2021 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francis kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es salaam na Askofu wa heshima wa Jimbo la Dar es Salaam.

Tarehe 07 Machi 2025 Baba Mtakatifu amteua kuwa Askofu wa kwanza Jimbo Jipya la Bagamoyo