Dar es Salaam
Usaidizi wa Wateja
"Jubilei ya miaka 75 ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam - Tufanywe upya na Roho Mtakatifu
Kardinali Laurian Rugambwa alizaliwa Tar 12 Julai 1912 katika kijiji cha Bukongo Parokia ya Rutabo - Kamachumu Jimbo Katoliki la Bukoba huko Kagera, Tanzania. Baba yake aliitwa Domitian Rushubirwa na mama yake Asteria Rushubirwa Mukaboshezi. Alipewa Jina Rugambwa ikimaanisha " anayenenewa vizuri au anayejulikana au mtukuka".
Alibatizwa na padre mmisionari wa Afrika, Padre Emil Verfurth Tar 21 Machi 1921 katika Parokia ya Kagondo,
Alisoma shule ya msingi hadi darasa la nne hapo Rutabo, 1926 alijiunga na Seminari ndogo ya Rubya mpaka 1933. Baadaye alitumwa Seminari Kuu ya Katigondo Uganda kwa masomo ya Falsafa na Teolojia, katika Seminari zote alifundishwa na Wamisionari wa Afrika walioinjilisha Tanzania Magharibi na Uganda Kusini.
Alipadrishwa Tar 12 Desemba1943 na Askofu Burchard Huwiler huko Parokia ya Rutabo Vikariati ya ya Bukoba akiwa na umri wa Miaka 31, baada ya Upadrisho alipangiwa utume wake kwenye Parokia ya Kagondo na baadae Parokia ya Ruby, mwishowe alihamishiwa Parokia ya Kashozi ambayo ni Parokia ya kwanza kuanzishwa Kagera.
Padre Laurian Rugambwa alitumwa Roma kwenye Chuo Cha Kipapa cha Urbamana kusomea shahada ya uzamivu katika Sheria za kanisa (Canon Law) na kufuzu. 13 Desemba 1951 aliteuliwa kuwa Askofu Mwafrika wa kwanza na Baba Mtakatifu Pio XII[ Vikariati ya Kagera] na baadaye alipewa Daraja Takatifu ya Uaskofu Tar 10 Februari 1952 na kukabidhiwa Parokia tano zilizokuwa kwenye Vikariati ya Kagera Ndogo.
Tarehe 28 Machi 1960 Papa Yohane wa XXIII alimteua Mhashamu Laurian Rugambwa kuwa Kardinali wa Kwanza Mwafrika na tena Mwafrika mweusi, hii ilikuwa heshima kubwa sana katika historia ya Kanisa. Nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania hazikuwa zimepata uhuru na mtu mweusi sehemu nyingi alidharauliwa, ni kipindi ambapo wengi walipata mshangao wasijuwe imewezekanaje, maana ni katika wakati majimbo karibia yote ya Tanganyika yalikuwa chini ya wamisionari Wazungu, haikuwa rahisi kufikiria Mwafrika kuwa Kardinali maana kwa wakati huo hadhi hiyo ilikuwa juu mno. Hata kwa wakati huo ukoloni ulikuwa bado umekolea mno na Waafrika bado walikuwa wakijihisi wanyonge na tena duni, wakati huo pia 1960, TANU ilikuwa imepamba moto kupigania uhuru chini ya uongozi wa Mwl. Julius K. Nyerere. Katika watu mashuhuri wa Afrika, Mwadhama alikuwa miongoni mwa waliopewa hadhi hiyo akilinganishwa na mashujaa wa Afrika ya dhama zile, lakini tunaamini ilikuwa ni mapenzi ya Mungu kwa watu wake. Baada ya kukabidhiwa Vikariati ya Kagera, alianza kutekeleza majukumu mbalimbali kama ifuatavyo;
Alijenga Kanisa Kuu mjini Bukoba, alipanua shule na hospitali zilizokuwepo na kujenga mpya mfano, alijenga Seminari Kuu ya Ntungamo 1967, alijenga Sekondari kubwa na nzuri ya wasichana ya Rugambwa kwa msaada kutoka Ujerumani, alipanua sekondari ya Ihunga, Chuo cha ualimu Kajunguti na Kuboresha Shule nyingi za msingi.
Desemba 19. 1968 alihamishwa toka Bukoba na kuwa Askofu Mkuu wa kwanza Mwafrika wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kushika nafasi ya Askofu Mkuu Edgar Maranta aliyeongoza kwa miaka 39. Alifika Dar es Salaam Tar 19 Mei 1969. Aliongoza kama Askofu Mkuu kwa Miaka 23. Alistaafu akiwa na umri wa Miaka 80. Alifariki Dunia Tar 8 Desemba 1997 na kutolewa heshima Kanisa Kuu la Dar es Salaam na Mwanza, alizikwa Parokia ya Rutabo 1997
Wakati anakabidhiwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Tar 25 Mei, 1969, parokia zilikuwa saba tu, Mapadre wa Jimbo walikuwa wawili tu, wengine wote walikuwa Wanashirika Wakapuchini. si.
Baraza la Maaskofu (Tanzaia Episcople Conference) lilianzishwa Mwaka 1956 waanzilishi akiwemo Kardinali, Rugambwa, Mwafrika pekee ambaye pia alikuwa mwasisi miongoni mwa wazungu waliopo kwenye Baraza hilo.
alijenga Semianari Kuu ndani ya Dar ea Salaam ili kukuza miito na kupata makasisi zaidi kukidhi mahitaji ya majimbo ya Tanzania, Seminari Kuu ya Mt. Karoli Lwanga -Segerea ilijengwa mwaka 1979. Alijenga pia Seminari Ndogo ya Saint Marys Visiga na mwaka 1990 ilifunguliwa.
Alianzisha Shirika la Dada Wadogo wa Mt. Fransisko wa Asizi 1983. Mwaka 1987 Watawa waliweka nadhiri zao za kwanza. Makao yao yakiwa Mbagala.
Baada ya Serekali kuamua kutaifisha zahanati iliyokuwa ikiendeshwa na Masista wa Mt. Fransisko iliyokuwepo Pugu 1970, Kardinali alipenda kuwa na hospitali ya Jimbo hivyo basi, akishauriana na viongozi wa jimbo, aliomba kubadilishana na zahanati ya serikali iliyopo Ukonga Tar 22 Mei 1986, Ariadina Bijuka alikabidhiwa uongozi wa zahanati ya Ukonga.
Mbali ya huduma zilizokuwa zinatolewa, kituo kiliendelea kuboreshwa siku hadi siku. Tar 14 Machi 1989 serikali ilikabidhi jengo la zahanati vifaa vyote na wafanyakiazi kwa kanisa. Makabidhiano yalifanyika chini ya Msgr Deogratias Mbiku kwa idhini ya Kardinali.
Tarehe 20 Machi 1989 ukarabati na ujenzi wa majengo mbalimbali chini ya Padre Zacheo ulianza. Ndio leo inayojulikana kama hospitali ya Kardinali Rugambwa